Mganga mkuu wa Mkoa wa Tanga Jonathan Budenu akiongea jambo na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Omary Mgumba kwenye kikao cha lishe cha Mkoa.
Wajumbe wa kikao cha lishe cha Mkoa huo, wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Mgumba akiongea na wajumbe wa kikao cha lishe cha Mkoa wa Tanga
*************************
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Jonathan Budenu ametakiwa kuhakikisha anaweka utaratibu wa kuweka mabango ya aina ya vyakula vinavyotakiwa kutumiwa na wakina mama wajawazito ili kuweza kujifungua watoto wenye afya njema na kuondoka tatizo la ugonjwa wa udumavu kwa watoto hao.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba wakati wa kikao cha lishe cha Mkoa huo ambapo alizitaka halmashauri kufuatilia idadi ya watoto wenye ugonjwa wa udumavu na kwamba mtoto anatakiwa awe na afya njema kuanzia akiwa tumboni kwa mama yake, hivyo anatakiwa kupatiwa kinga kabla hajazaliwa..
Mgumba amesema Mkoa wa Tanga umekuwa na ongezeko la asilimia 2 la ugonjwa wa udumavu kwa kuwa na asilimia 34 na kuzidi ya Kitaifa inayotakiwa ambayo ni asilimia 32.
"Taarifa za lishe, ulaji mzuri wa vyakula zibandikwe kwenye mbao za matangazo katika ofisi zote za taasisi za serikali katika ngazi zote za kitongoji, kijiji, kata, Wilaya mpaka Mkoa, lakini tuangalie aina ya vyakula vinavyopatikana kwenye eneo husika" amesema Mgumba.
"Kinga ni bora kuliko tiba, na hakuna maradhi mabaya kama ya udumavu na ndiyo maana tunaambiwa mtoto anyonyeshwe mpaka miaka miwili na apewe lishe bora ili kumkinga na huu udumavu, wazazi tunazunguuka sana watoto wetu wanapokuwa na ulemavu lakini ulemavu mmbaya ni udumavu wa akili" amesisitiza.
Aidha Mgumba amezitaka halmashauri zote za Mkoa huo kutenga fedha za lishe kwa watoto wadogo kupitia mkataba uliopo na kuzitumia kwa matumizi yaliyopangwa ili na siyo kutumia kinyume na matumizi husika.
"Kuna halmashauri ambazo hazichangii fedha kwa ajili ya watoto kiasi cha sh 1000 kwa kila mtoto, wakati zingine zinachangia lakini hazifikii kiasi kilichopangwa na pia zipo zinazochangia zote na kuzitumia fedha hizo katika miradi mingine, hili ni tatizo, fedha zinazotengwa za watoto zifanyie kazi yake" amesema.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Pili Mnyema amesema kutokana na halmashauri hizo kusuasua katika kutenga fedha za watoto, kuna haja ya serikali kusimamia kwa dhati kuhakikisha inazisimamia ili kuweza kutimiza malengo yaliyowekwa.
"Tathimini za takwimu za uhalisia zilizofanywa na Wizara zimeonesha kuwa katika Mkoa huo zipo Wilaya ambazo zimefanya vizuri lakini pia Wilaya moja ya Kilindi imeshika nafasi ya mwisho kwa kushindwa kufikia malengo ya kutenga fedha kwa asilimia 100" amesema.
Ofisa lishe Mkoa wa Tanga Mwanamvua Zuberi amesema watoto wanapata udumavu ni chini ya miaka mitano huku akitoa mchanganuo wa viashiria vya ugonjwa huo, "kuna viashiria vingi ambavyo vimeonesha watoto waliopo chini ya umri wa miaka mitano waliotumia ni asilimia 34, lakini asilimia 2.7 wana ukondefu na asilimia 15.6 wana uzito pungufu" amefafanua.
Pia amebainisha kwamba wanafanya jitihada za kuogeza viashiria vya lishe kwa kutoa huduma mbalimbali za kitabibu ikiwemo ya utapiamlo lakini pia kuhakikisha wanafanya utekelezaji wa mkataba wa lishe pamoja na kufanya ufuatiliaji katika vituo vyao vyote vya kutolea huduma.
"Tunatoa pia vidonge vya wekundu wa damu kwa wakina mama wajawajazito, kwa sababu wanaweza wakapungukiwa na damu mjamzito akipungukiwa na damu mara inaweza kupelekea kujifungua mtoto mwenye damu pungufu, na pia tunashirikiana na kutoa elimu ngazi ya jamii" ameeleza.
0 Comments