Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI WA USAFIRISHAJI ZAMBIA AFANYA ZIARA BANDARI, TAZARA

Na Mwandishi Wetu, Dar

Waziri wa Uchukuzi na Usafirishaji wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Frank Tayali amefanya ziara ya kutembelea Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Kampuni binafsi ya Kimataifa ya Kuhudumia Makontena Tanzania (TICTS) pamoja na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) Jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo Mhe. Tayali aliambatana na mwenyeji wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (Mb) ambapo pamoja na mambo mengine, viongozi hao wametembelea maeneo hayo ikiwa ni siku moja tu tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema walipowaelekeza Mawaziri wa Sekta hiyo kushughulika changamoto zinazoikabilia miundombinu ya kiuchumi baina ya nchi hizo ikiwemo reli ya Tazara na Bomba la mafuta la Tazama.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amemhakikishia Waziri mwenzake kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Zambia katika kutafuta mikakati ya kuifufua reli ya Tazara na kuhakikisha kuwa wafanyabishara kutoka Tanzania na Zambia wananufaika na reli ya Tazara.

“Tanzania na Zambia ni washirika na ndugu hivyo sisi kama watanzania tupo hapa kuwahudumia na pia tupo tayari kushirikiana nanyi kuhakikisha kuwa uchumi wetu unakua……………. kupanua wigo wa biashara baina ya mataifa yetu,” amesema Prof. Mbarawa.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Bw. Plasduce Mbossa amesema kuwa Zambia ni nchi moja wapo kati ya nchi zainazotumia Bandari ya Tanzania kwa asilimia kubwa ambapo Bandari inatambua mchango mkubwa wa wafanyabiashara kutoka Zambia wanavyotumia bandari ya Tanzania na kuwa Bandari inawaahidi ushirikiano katika kukuza na kuendeleza biashara baina ya Tanzania na Malawi.

Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi na Usafirishaji wa Zambia, Mhe. Tayali amesema Tazara ni nyenzo muhimu katika kuinua uchumi wa mataifa yote mawili, hivyo kufufuliwa kwa reli ya Tazara kutasaidia kuinua uchumi wa mataifa yote hususan kwa wafanyabiashara na wawekezaji.

“Zambia tutafanya kazi kwa bidii kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutafuta mikakati mbalimbali ya kuifufua Tazara ili kuendelea kunufaisha watanzania na wazambia kwani bila kufanya hivyo maendeleo ya mataifa hayo yatadhorora,” amesema Mhe. Tayali

Aidha, viongozi hao wamewaagiza Makatibu Wakuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kutoka Tanzania na Zambia kushirikiana na Uongozi wa Tazara kuunda Kamati ya kufuatilia mikakati ya ufufuaji wa Reli ya Tazara mapema iwezekananyo ili kuanza kutekeleza maagizo ya viongozi wakuu wa nchi yaliyotolewa jana tarehe 2 Aug, 2022 wakati wa Ziara rasmi ya kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Zambia nchini Tanzania jana.


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (kulia) na mgeni wake Waziri wa Uchukuzi na Usafirishaji wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Frank Tayali (kushoto) wakichukua dondoo walipofanya ziara katika Mamlaka ya Bandari Tanzania. Mhe. Tayali ametembelea bandari ya Tanzania kwa lengo la kujionea jinsi bandari hiyo inavyotekeleza majukumu yake


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa na mgeni wake Waziri wa Uchukuzi na Usafirishaji wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Frank Tayali wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) Mhandisi Bruno Tching'andu (aliyesimama) alipokuwa akieleza jinsi Tazara inavyotekeleza majukumu yake





Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa na mgeni wake Waziri wa Uchukuzi na Usafirishaji wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Frank Tayali wakipata taarifa fupi kuhusu Kampuni binafsi ya Kimataifa ya Kuhudumia Makontena Tanzania (TICTS) inavyotekeleza majukumu yake wakati walipotembelea ofisi za TICTS Jijini Dar es Salaam


Kikao cha Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa na mgeni wake Waziri wa Uchukuzi na Usafirishaji wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Frank Tayali kikiendelea katika Ofisi za Tazara Jijini Dar es Salaam

Post a Comment

0 Comments