Ticker

6/recent/ticker-posts

VYAMA VYA USHIRIKA VYATAKIWA KUWA MKOMBOZI WA WAKULIMA, WAFUGAJI NA WAVUVI


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na viongozi na wananchi kwenye siku ya Mifugo na Uvuvi ya Maadhimisho ya Wiki ya Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini kwenye Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi, ambapo amewasihi wafugaji na wavuvi kujiujiunga kwenye vyama vya ushirika na kuwataka wananchi kutumia mazao ya mifugo na uvuvi.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (wa nne kutoka kushoto) akisikiliza maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo na Utafiti kutoka Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), Bi. Eileen Nkondola (wa sita kutoka kushoto) kuhusu bwawa linalohamishika kwenye Banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo kwenye Viwanja vya Maonesho ya Nanenane – Ngongo Mkoani Lindi.


Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Mhe. Judith Nguli akito salamu za mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi wakati wa siku ya Mifugo na Uvuvi ya Maadhimisho ya Wiki ya Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini kwenye Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.


Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo, Dkt. Erastus Mosha akiwashukuru viongozi wa Kanda ya kusini kwa maandalizi mazuri waliyoyafanya kwa kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanapata fursa kubwa kupitia maonesho ya Nanenane kukutana na wadau mbalimbali kwenye mnyororo wa thamani wa mazao yao.


Mkurugenzi Msaidizi Utafiti na Mafunzo, Dkt. Hassan Mruttu akitoa salamu za Sekta ya Mifugo wakati wa siku ya Mifugo na Uvuvi ya Maadhimisho ya Wiki ya Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini kwenye Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiangalia viatu vya ngozi katika Banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini kwenye Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi. Kulia ni mfanyabiashara wa bidhaa za ngozi, Bw. Suleiman Hassani


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akizungumza wakati alipotembelea banda la Chama cha Ushirika cha TANECU kwenye siku ya Mifugo na Uvuvi ya Maadhimisho ya Wiki ya Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini kwenye Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akisalimiana na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Lindi mara baada ya kuwasili mkoani hapo kwa ajili ya siku ya Mifugo na Uvuvi ya Maadhimisho ya Wiki ya Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini kwenye Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akimuangalia ng’ombe aliyemkuta kwenye banda la Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwenye Maonesho ya Nanenane – Ngongo mkoani Lindi.

......................................

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amevitaka Vyama vya Ushirika vya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi nchini kuwa msaada katika kuleta maendeleo na sio kushiriki kushusha maendeleo ya wadau wa sekta hizo.

Naibu Waziri Ulega ameyasema hayo wakati wa siku ya Mifugo na Uvuvi ya Maadhimisho ya Wiki ya Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini kwenye Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi, ambapo amesema lengo la kuanzishwa kwa ushirika ni kuwasaidia wanyonge kuwa na nguvu moja itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Vyama vya Ushirika ni muhimu kwa wafugaji na wavuvi kwani vinasaidia kuwakutanisha pamoja ambapo wataweza kupata fursa mbalimbali zikiwemo za mikopo na bima. Wizara inaendelea kuwahamasisha wafugaji na wavuvi kujiunga kwenye vyama vya ushirika kwa kuwa ni njia ambayo itawafanya wawe na nguvu moja kwenye maamuzi ya biashara ya mazao yao.

Naibu Waziri Ulega pia amewataka viongozi wa Vyama vya Ushirika kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kwani kumekuwepo na malalamiko mengi kwenye baadhi ya vyama kutokana na ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji kitu kinachosababisha wakulima, wafugaji na wavuvi kuilalamikia serikali.

Vilevile ameendelea kuwasihi wananchi kutumia mazao yatokanayo na mifugo na uvuvi kwa kuwa ni muhimu katika kujenga na kuimarisha afya. Pia amewashauri watanzania kuendele kutumia bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao la ngozi kama viatu, mikanda na mikoba kwa kuwa bidhaa hizo ni bora na zinazalishwa hapa nchini.

Naibu Waziri Ulega amewasihi wafugaji kuhakikisha wanavisha hereni za kielektroniki kwenye mifugo yao kama taratibu zinavyotaka kwa kuwa mfumo huo una faida kubwa. Serikali inaendelea na uboreshaji wa mazingira ya wafugaji kwa ujenzi wa majosho, malambo na uhamasishaji wa utunzaji wa nyanda za malisho na kilimo cha malisho ya mifugo ili wakati wa kiangazi wafugaji wasiweze kupata tabu. Pamoja na mambo mengine kwa mkoa wa Lindi, Wizara inajenga Malambo kwenye Kijiji cha Kimambi (Wilayani Liwale) na Matekwe (Wilayani Nachingwea) ili wafugaji waweze kupata maji ya kunyweshea mifugo yao.

Aidha, amesema Wizara hiyo inakusudia kuanza kutoa mikopo kwa vifaa kwa wavuvi ili waendeleze shughuli zao na hatimaye kuinuka kiuchumi, ambapo pia amesema zipo boti 250 za kisasa ambazo zitakopeshwa kwa wavuvi. Huku akibainisha kwamba kipindi kirefu wavuvi wamekuwa wakitumia zana duni za uvuvi na hivyo kuvua kwa kubahatisha lakini sasa serikali imedhamiria kumsaidia mvuvi kuhakikisha anakwenda kuvua eneo ambalo samaki wanapatikana.

Pia Naibu Waziri Ulega amewataka viongozi wa vijiji kuhakikisha wanasimamia Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ili maeneo yanayotengwa kwa ajili ya shughuli za mifugo zisiweze kuingiliwa na watumiaji wengine wa ardhi. Lakini pia amewasihi wafugaji kuto lisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima kwa kuwa hiyo ni moja ya chanzo cha migogoro na ikitokea tukio kama hilo serikali itachukua hatua.

”Wakulima na Wafugaji ni ndugu kwa kuwa wote wanategemeana, hivyo ni vyema kila mmoja akaiheshimu kazi anayoifanya mwenzake ili wote kwa pamoja waweze kuendelea na kujiingizia kipato kutokana na shughuli wanazofanya,” alisema Naibu Waziri Ulega

Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Mhe. Judith Nguli amesema kuwa kupitia elimu inayotolewa kwenye maonesho ya nanenane anaamini wakulima, wafugaji na wavuvi watakwenda kutumia mbinu za kisasa kwenye shughuli wanazofanya, kitu ambacho kitawasaidia kuongeza tija katika uzalishaji na biashara ya mazao hayo.

Kwa upande wake Dkt Hasan Mruttu Mkurugenzi Msaidizi Utafiti na Mafunzo amezishauri Halmashauri kuendelea kuwahamasisha wafugaji na wavuvi kujiunga kwenye vyama vya vyama vya ushirika ili viwasaidie katika kutetea maslai yao.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo, Dkt. Erastus Mosha amewashukuru viongozi wa Kanda ya kusini kwa maandalizi mazuri waliyoyafanya kwa kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanapata fursa kubwa kupitia maonesho hayo kukutana na wadau mbalimbali kwenye mnyororo wa thamani wa mazao yao.

Post a Comment

0 Comments