*******************
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) wamepongeza uwekezaji mkubwa kwenye tasnia ya Maziwa Nchini uliofanywa na kiwanda cha 'Asas Dairies' kilichopo Mkoani Iringa.
Wajumbe hao wameipongeza Kampuni ya kuchakata Maziwa ya Asass kwa uwekezaji huo mkubwa walipofika kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Kampuni hiyo kwa upande wa Sekta ya Maziwa Mkoani humo walipotembelea Agosti 29 na 30,2022.
Akitoa neno la shukrani mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea shamba la Asas, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Bodi ya Maziwa Profesa Zacharia Masanyiwa ameusifu uwekezaji mkubwa uliofanywa na Kampuni hiyo ya uzalishaji wa Maziwa ambao umeonesha maana halisi ya ufugaji kibiashara.
"Kwanza niwashukuru sana kwa mapokezi mazuri na ziara nzuri yenye manufaa kwetu, lakini pia niseme leo nimeona maana halisi ya ufugaji kibiashara kupitia uwekezaji huu mkubwa ." Amesema Prof. Masanyiwa.
Pia Profesa Masanyiwa amewataka wadau hao wa Maziwa nchini kuendelea kushirikiana na Bodi ya Maziwa Tanzania kwani ndio wasimamizi Wakuu wa Tasnia hii Nchini.
"Ninawapongeza sana lakini niwaombe kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu sana na Bodi ya Maziwa Tanzania, Bodi sio mshindani wenu bali ni mshirika wenu katika kuendeleza sekta hii muhimu."
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Dkt. George Msalya amesema ziara hiyo imekuwa ya umuhimu sana kwa Wajumbe wa Bodi ya Ushauri katika kuijua vizuri Tasnia ya Maziwa.
"Lengo la ziara hii ni kuwapatia wajumbe wa Bodi nafasi ya kuijua vizuri Tasnia ya Maziwa na uwekezaji mkubwa unaofanywa na wadau katika sekta hii muhimu Nchini."
Naye Bw. Athumani Mahadhi ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Bodi hiyo amezungumzia kuimarika kwa ushirikiano kati ya wawekezaji wa Sekta binafsi na Serikali.
"Kusema ukweli siku hizi mambo yamebadilika sana tofauti na zamani, zamani wawekezaji walikuwa wagumu sana kuruhusu kuona teknolojia wanayoitumia lakini leo tumejionea Asas wametupitisha sehemu yote ya shamba na kiwanda na kuona teknolojia wanazotumia." Amesema Bwana Mahadhi.
Naye Maneja Masoko wa Asas Dairies Bw. Mtimila Lipita ameishukuru Bodi ya Maziwa Tanzania kwa kutembelea kiwandani hapo na kuona shughuli zinazofanywa shambani na kiwandani.
0 Comments