Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YAJIPATIA MEDALI 22 KWENYE MICHEZO YA JUMUIYA YA MADOLA


Bondia Kassim Selemani Mbundwike akipambana kishujaa na bondia Tiago Osorio Muxanga wa Msumbiji katika nusu finali ya pili ya uzani wa 67kg-71kg (Light Middle) katika Ukumbi wa NEC jijini Birmingham, Uingereza. Hata hivyo alipoteza pambano kwa kuzidiwa pointi.

*********

Na Issa Michuzi, Birmingham

Tanzania imehitimisha ushiriki wake katika Michezo ya 22 ya Jumuiya ya Madola jijini Birmingham, Uingereza, ikiwa katika nafasi ya 28 baada ya mategemeo yake manne ya mwisho kushindwa kuambulia chochote kwenye michezo yao usiku wa kuamkia leo.

Kwanza alianza bondia Yusuf Lucasi Changalawe kwa kupambana na Sean Lazzerini wa Scotland katika nusu finali ya kwanza ya uzani wa 75kg-80kg (Light Heavyweight ) katika Ukumbi Namba 4 wa National Exhibition Centre (NEC) ambapo alishindwa kwa pointi.

Tegemeo la pili lilikuwa kwa bondia Kassim Selemani Mbundwike aliyepambana kishujaa na bondia Tiago Osorio Muxanga wa Msumbiji katika nusu finali ya pili ya uzani wa 67kg-71kg (Light Middle) katika Ukumbi huo huo, lakini naye akazidiwa pointi.

Hata hivyo, kwa mabondia Changalawe na Mbundwike kucheza hatua hiyo ya nusu finali imemaanisha kwamba kila mmoja wao tayari ana medali ya Shaba, kwani katika ndondi mabondia wote wanaofika hatua hiyo huwa moja kwa moja wanatunukiwa medali hiyo, hata kama watashindwa katika mchezo wao wa nusu fainali.

Karata zingine mbili zilizosalia walikuwa nazo wanariadha Josephat Joshua Gisemo na mwenzie Faraja Lazaro Damasi ambao walikimbia bega kwa bega katika dimba moja katika fainali ya mbio za mita 5,000 Uwanja wa Alexander, wakikwa miongoni mwa wanariadha 20 kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola waliowania medali za Dhahabu, Fedha na Shaba.

Pamoja na juhudi kubwa walizofanya lakini Watanzania hawa walimaliza katika nafasi za 15 na 16, huku Jacob Kiplimo wa Uganda akishika nafasi ya kwanza akifuatiwa na Wakenya N. Kimeli aliyebeba medali ya Fedha na J. Kiprop akiondoka na medali ya Shaba.

Hivyo kimsimamo hadi leo asubuhi Tanzania inashika Nafasi ya 28 katika ambazo zimeambulia medali. Takriban wanamichezo 5,054 wanashiriki katika Michezo hiyo kutoka Nchi 72 ambapo jumla ya michezo 20 huchezwa.

Jirani zetu Kenya ni wa 12 kimsimamo hadi jana kwa kuwa na jumla ya medali 16 ikiwa ni 4 za dhahabu, 5 za Fedha na 7 za Shaba. Uganda ni ya 13 kwa kuwa na Medali tatu za Dhahabu na mbili za Shaba.

Bara la Afrika linaongozwa kimsimamo na Nigeria na Afrika ya Kusini katika kupata medali nyingi ambapo hadi leo asubuhi Nigeria ni wa 6 kimsimamo kwa kupata jumla ya medali 16, ambapo 9 ni Dhahabu, 8 ni Fedha na 13 ni Shaba.

Afrika ya Kusini hadi asubuhi hii kimsimamo ni ya 7 kwa kunyakua jumla ya medali 7 za Dhahabu, 8 za Fedha na 11 za Shaba.

Hadi leo asubuhi nchi inayoongoza kwa wingi wa medali ni Australia yenye jumla ya medali 155, ambazo ni dhahahu 59, Fedha 46 na Shaba 50. Hao Wanafuatiwa na wenyeji Uingereza ambao hadi asubuhi hii walikuwa na kumla ya medali 148 kiwa ni dhahabu 50, Fedha 52 na Shaba 46.

Hadi sasa Tanzania imeweza kujipatia jumla ya medali 22 (zote katika riadha na ndondi) katika Michezo hio ya Jumuiya ya Madola ambayo nchi imeshiriki michuano yote tokea ipate Uhuru isipokuwa Mwaka 1968,

Katika medali hizo 22, hadi leo Tanzania imeshinda 6 za Dhahabu, 7 za Fedha na 9 za Shaba.


Wakati huo huo, rekodi ya riadha ya Tanzania ambayo haikuwahi kuvunjwa ya mbio za mita 1,500 iliyowekwa Mwaka 1974 na Filbert Bayi jijini Christchurch, New Zealand, imevunjwa jana na mkimbiaji wa Australia Oliver Hoare kwa muda wa dakika 3:30.12

Post a Comment

0 Comments