Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, akitazama ndege isiyo na rubani (drone) katika banda la Bodi ya Sukari katika maonyesho ya kilimo (Nanenane) mkoani Morogoro.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, akiwa katika baadhi ya mabanda yanayoshiriki maonyesho ya kilimo (Nanenane) mkoani Morogoro. (PICHA NA CCM MAKAO MAKUU
***************************
Na Mwandishi Wetu ,Morogoro
KATIBU wa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka ametoa muelekeo wa kutatua changamoto ya ajira kwa vijana nchini hasa wasomi wa vyuo vikuu huku akitaka wasomi hao watambuliwe na kisha wawezeshwe na hatimaye kujajiri.
Shaka alitoa muelekeo huo jana alipofanya ziara ya kutembelea Maonesho ya Kilimo maarufu Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika mkoani Morogoro ambapo alisema kwenye maonesho hayo liko jambo la faraja ambalo ameliona.
“Kupitia maonesho haya mimi kwangu naona ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan anaelekea kufanikiwa kwa namna ambavyo vijana wameamua kuwekeza katika sekta hii ya kilimo.
“Tumewatembelea vijana wadogo ambao wote na kila mmoja ameweza kutafsiri maono ya Rais kwa aidha kwa kufikiria kuanzisha kitengo cha kuwasaidia vijana wenzake au kuwekeza kwenye masuala haya ya kilimo
“Na kwenye hili mimi nitoe mwito kwa Wizara ya Kilimo na Serikali, tumembelea taasisi za kifedha wameonesha utayari wao sasa pamoja na kwamba Rais ametenga bajeti kubwa kwa ajili ya kilimo nadhan iko haja ya kuweka mipango mizuri na madhubuti ili fedha hizi zinazotengwa na taasisi hizo za kifedha.
“Nazo pia ziweze kutiliwa mkazo na mtazamo maalum kwa kuyanufaisha makundi ambayo nimeyasema.Kwa mkoa huu wa Morogoro uko mfano mzuri sana tunacho Chuo cha Kilimo Morogoro.
“Nadhani tukiwekeza pale kwani kila mwaka vijana wanahitimu , hivyo nadhani tukiwekeza kwanza kuwa na takwimu sahihi za vijana wangapi wanahitimu lakini pia kuwatambua hao vijana maeneo wanayotoka kisha Serikali ikatenga maeneo maalum kila kijana ikampa wastani wa heka japo tano,”alisema Shaka.
Aliongeza baada ya kutengwa maeneo maalumu na mashirika ya fedha nayo yakatoa fedha kwa vijana hao na anaamini kwa changamoto ya ajira iliyopo wanaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa.
“Hilo linawezekana na tujifunze nchini Misri ambao wenzetu wameweza kwa njiia kama hiyo na sisi Tanzania tunaweza zaidi ya hapo lakini lazima kuwe na mipango madhubuti ya kuhakikisha vijana hawa tunawaandaa tangia wanamaliza au wanahitimu vyuo vikuu hadi wanaingia kwenye soko la ajira,”alisema.
Shaka alisema kwenye maonesho ya Nanenane mwaka huu ameiona dhamira ya Serikali kuuhuisha na kuunganisha vijana kutumia sekta ya kilimo kama mkombozi katika kujenga uchumi.
Aidha alisema lingine ambalo analiona kwenye suala la kilimo lazima waambizane na wawe tayari lakisi sio kuwa tayari tu wakati umefika sasa Watanzania kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ili kuweza kufanya kilimo chetu vizuri.
Katika hatua nyingine Shaka alisema kwenye maonesho ya mwaka huu ameshudia mabadiliko na maboresho makubwa na yote yanaonesha utayari wa viongozi katika kutafsiri dhana na dhima waliyonayo kwa vitendo ya kusimamia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kwa mwaka huu yapo mambo kadhaa tumejifunza nadhani tunafahamu kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa letu lakini tunafahamu kilimo tunakitegemea kwa asilimia 70 ndani ya nchi yetu katika kuendesha maisha yetu ya kila siku lakini pia kunyanyua uchumi wa nchi yetu.
“Sasa kwa mwaka huu tunaongozwa na dhamira ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko katika sekta hii ya kilimo, wote tumeshuhudia ukitaka kutafsiri na kujua namna gani ambavyo Rais anaitazama sekta ya kilimo kama mkombozi kwa watanzania namna ambavyo ameweza kufanya mabadiliko makubwa,”alisema.
Aliongeza hata baada ya uhuru wa nchi hii haijapata kutokea bajeti ya mwaka 2022/2023 Rais Samia ametenga fedha karibia Sh.bilioni 954 ukingalisha na bajeti ya mwaka 2021/2022 ya Sh.bilioni 254 karibia asilimia 224 ya ongezeko hilo la bajeti.
“Lengo kuonesha mkazo zaidi katika Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza nguvu huko na dhamira kubwa ikiwa kuwaomboa vijana pamoja na wanawake.
“Katika hilo Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi imeahidi katika kipindi cha miaka mitano tutazalisha ajira milioni nane kwa watanzania , sasa kwenye kutafsiri maelekezo ya Ilani Serikali ya Rais imeshajiwekea muekelekeo ama imeshajiwekea matatarajio yake katika ajira hizo,”alisema Shaka.
Alifafanua Serikali inatarajia mpaka kufikia 2025 karibia ajira milioni tatu zitakuwa zimezalishwa kupitia sekta hii ya kilimo huku akiongeza hayo ni mageuzi makubwa na huo ni ukombozi kwa vijana na wanawake.
0 Comments