Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la World Vision nchini Filbert Komanga katikati, anayefuata kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Save the Children Bester Malauzi.Mkuu wa Mkoa katikati akikata utepe kama ishara ya kuzindua mradi huo.
mkuu wa Mkoa akimkabidhi ndoo ya mafuta mkuu wa Wilaya ya Handeni Siriel Mchembe kama ishara ya kumkabidhi vyakula waliyopatiwa na mashirika hayo.
Wanafunzi wa shule za msingi Wilaya ya Mkinga ambao wamenufaika na mradi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba akiongea na wananchi kabla ya kuzindua mradi huo.
***********************
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
TATHIMINI ya usalama wa chakula nchini imeonesha kwamba Wilaya mbili za Mkoa wa Tanga ziko kwenye hatari ya usalama mdogo wa chakula na hii ni kutokana na upungufu mkubwa wa chakula katika ngazi za kaya.
Kupitia hali hiyo Shirika la World Vision kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Save the Children yamejipanga kusaidiana na serikali katika mpango wa upatikanaji wa chakula mashuleni na wamezindua rasmi juzi katika jitihada za kupunguza athari za ukame wa muda mrefu.
Akiongea kabla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la World Vision nchini Filbert Komanga amesema wamezindua mpango huo wenye thamani ya zaidi ya sh milioni 597 katika shule 54 za msingi katika Wilaya za Mkinga na Handeni.
"Mpango huu unategemea kuwafikia watoto 28, 110 katika shule hizo kwa kipindi cha miezi mitatu, kuanzia Septemba mpaka Novemba 2022, kwa lengo la kupunguza athari za ukame wa muda mrefu uliozikumba Wilaya hizo" amesema.
"Kwa kugawa chakula mashuleni ambapo watoto watakuwa na uhakika wa kupata mlo wa asubuhi na mchana wawapo shuleni, ugawaji huu unalenga kuinua ufaulu na kuongeza mahudhurio yao shuleni, lakini pia kuwasaifdia wazazi kupambana na upungufu wa chakula majumbani kwani huathiri mahudhurio ya watoto pamoja na kipato cha familia" ameongeza Komanga.
Aidha amefafanua kuwa kwa Wilaya ya Mkinga zipo shule 30 zenye wanafunzi 13, 421 ambapo wamepatiwa kilo 70, 697 za mahindi, kilo 39, 276 za maharagwe, kilo 2, 357 za chumvi na ndio za lita 20 za mafuta ya kula zipatazo 393, vyenye thamani ya sh milioni 216, 439, 900.
Komanga amebainisha kwamba kwa Wilaya ya Handeni zipo shule 24 ambazo zina jumla ya watoto 14, 689 ambao watanufaika na upatikanaji wa chakula hicho ambapo jumla ya kilo 129,000 za mahindi, kilo 53, 000 za maharagwe, kilo 3, 600 za chumvi na lita 9, 000 za mafuta ya kula vyote vikiwa na thamani ya sh milioni 381, 233, 400.
"Wito wangu, serikali na jamii kwa ujumla tuungane katika kuanzisha mpango endelevu wa chakula cha shuleni, kwasababu mpango uliopo sasa hivi tuliozindua ni wa miezi mitatu na haiwezi kuendelea kwa kipindi chote" amesema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Save the Children Bester Malauzi amesema wao wana majukumu makubwa mawili, katika kuwezeshwa maendeleo lakini pia kuitikia pale inapotokea maafa katika eneo lolote.
Amesema ingawa hawana shuhuli nyingi kiuwajibikaji katika Mkoa wa Tanga, lakini walipoona Kuna viashiria vya usalama wa ukosefu wa chakula ndipo walipotafuta mdau wa kushirikiana naye ambaye ni Shirika la World Vision.
"Lengo hasa la mpango huu wa kugawa chakula cha watoto mashuleni ni kusaidia kabla hali haijakuwa mbaya zaidi, kwani hatuwezi kusubiria hali iwe hivyo ndio tuanze kusaidia, lakini pia tumeshafanya shuhuli mbalimbali za kusaidia katika ngazi ya kaya ili kuhakikisha usalama wa chakula" amesema Malauzi.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba amesisitiza kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanaendeleza mpango huo baada ya miezi mitatu kwisha ili kuweza kupunguza au kuondokana kabisa na suala la uhaba wa chakula na kuwafanya watoto waendelee kupata chakula mashuleni.
"Tuendelee kuchangia chakula mashuleni ili mradi huu usiwe mfu, wenzetu wamekuja kupanda mbegu, sisi tuendelee kupalilia na kuendelea mradi huu ambao wenzetu wameanza,
"Lakini pia viongozi wa halmashauri za Wilaya ya Mkinga na Handeni kuandaa wataalamu watakaotekeleza mradi huu kwa kipindi cha miezi mitatu ili tuwe na watu wenye uzoefu waliopata elimu jinsi ya kuendesha miradi hiyo katika halmashauri na Wilaya zetu na Mkoa wetu wa Tanga kwa ujumla" amesema.
Hata hivyo Mgumba ametoa msisitizo kwa jamii kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na maarifa ili kuunga mkono juhudi za serikali na kuongeza uzalishaji wa chakula na kipato uwe mzuri na kuweza kuhudumia familia zao lakini pia kuinua uchumi wa Taifa.
0 Comments