Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi wakishuhudia maadamano ya washiriki wa Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania ( UMISETA wakati alipozindua mashindano hayo kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, Agosti 4, 2022. Kulia ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul, wa tatu kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, David Silinde na wa nne kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi, Dkt. Batilda Burian. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Fazal Mohammed kutoka Tanga ambaye mchezaji wa mpira wa wavu wakati alipozindua Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISETA kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, Agosti 4, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISETA) kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, Agosti 4, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Katibu Mkuu, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbas nakala za vitabu vya miongozo na mikakati kwa ajili ya kuboresha elimu nchini inayolenga kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoathiri sekta ya elimu. Makabidhiano hayo yalifanyika wakati Waziri Mkuu alipozindua Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania ( UMISETA kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, Agosti 4, 2022. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, David Silinde.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua timu ya mpira wa miguu ya mkoa wa Ruvuma wakati alipozindua Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania ( UMISETA kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, Agosti 4, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inatambua mchango wa michezo shuleni, hivyo itaendelea kuhamasisha ufundishaji wa michezo katika shule za msingi na sekondari ili kuibua vipaji vipya vya michezo nchini.
Amesema katika kuwaandaa vijana kuwa na afya bora ya akili na mwili, Mheshimiwa Rais Samia ameahidi kuwa Serikali anayoiongoza itaendelea kuimarisha na kuongeza miundombinu ya shule pamoja na mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Alhamisi, Agosti 4, 2022) wakati akizindua mashindano ya Michezo na Taaluma kwa shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) wanafunzi, yanayofanyika katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mkoani Tabora.
“Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya michezo katika shule teule 56 nchini ikiwa ni wastani wa shule mbili kwa kila mkoa. Nimefurahi kuona utekelezaji wa mradi huu kwa mkoa wa Tabora tayari umeanza katika Shule za Sekondari Tabora Wavulana na Tabora Wasichana na viwanja vilivyojengwa vitatumika katika mashindano ya mwaka huu 2022.”
Amesema ujenzi wa miundombinu ya michezo utafanyika kwa awamu katika shule nyingine ili kuhakikisha kunakuwa na shule zenye miundombinu bora ya kuwezesha wanafunzi kusoma somo hilo kwa nadharia na vitendo. “Lengo ni kuzalisha wataalamu watakaobobea katika eneo hili la michezo.”
Amesema pamoja na ujenzi wa viwanja, Serikali itajenga kumbi kubwa katika shule hizo zitakazotumika kwa kazi za sanaa na michezo ya ndani. “Sambamba na hayo, Serikali imeendelea kuajiri walimu wa michezo ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 walimu wa michezo 83 wameajiriwa.”
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa michezo na utamaduni katika ukuaji na maendeleo ya wanafunzi kiakili na kijamii, kwa sababu michezo na sanaa ni miongoni mwa stadi muhimu zinazochangia ukuaji wa kiuchumi na kijamii ikiwemo kutengeneza fursa za ajira.
“Ni jukumu letu kuhakikisha kuwa tunajenga msingi imara wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa somo la elimu kwa michezo ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa vipaji vya michezo kwa wanafunzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari hadi vyuo vya elimu ya juu.”
Ili kufanikisha azma ya kuboresha michezo na taaluma nchini, Waziri Mkuu amewaelekeza viongozi wa elimu katika ngazi ya shule, kata, shehia, Halmashauri na Mkoa wafuatilie ufundishaji na ujifunzaji shuleni na kushauriana na walimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata umahiri uliokusudiwa kwa masomo yote badala ya kukaa muda mwingi ofisini.
“Kila mwalimu ahakikishe anajiwekea malengo yake binafsi katika masomo anayofundisha na kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayeshindwa kupata umahiri uliokusudiwa katika somo lake ifikapo mwishoni mwa kila mwaka.
Pia, Waziri Mkuu ameagiza uteuzi wa viongozi wanaopewa dhamana ya kusimamia Elimumsingi na Sekondari katika ngazi za Shule, Kata, Shehia, Halmashauri na Mkoa uzingatie umahiri, weledi, ubunifu na uzoefu kama ilivyobainishwa kwenye mwongozo waliouandaa.
Mbali na kufungua mashindano ya michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwa mwaka 2022, Waziri Mkuu pia amezindua vitabu vya miongozo na mikakati kwa ajili ya kuboresha elimu nchini inayolenga kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoathiri sekta ya elimu na kuongeza uelewa wa pamoja.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, David Silinde amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya kugharamia michezo hiyo na kwamba ofisi yake itahakikisha inafanyika kwa ufanisi mkubwa.
Naye, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul amesema katika kuhakikisha elimu kwa michezo inaendelea kutolewa vizuri shuleni Serikali imetenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya michezo.
0 Comments