*********************
Na Issa Michuzi, Birmingham
Michezo ya 22 ya Jumuiya ya Madola inafungwa rasmi leo katika Uwanja wa Alexander jijini Birmingham, Uingereza, huku jiji la Victoria, Australia, ndilo linalokabidhiwa mikoba kuandaa michuano ya 23 miaka minne ijayo.
Shamrashamra za kila aina zimeandaliwa kutumbuiza Mataifa 72 yaliyoshiriki mashindano hayo, zikiwemo burudani za Muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali wakubwa wa Uingereza, wakiwemo UB40 na waigizaji Dexys Midnight Runners watakaoonesha sehemu ya mchezo wao maarufu katika Peaky Binders: The Redemption of Thomas Shelby.
Tanzania inamaliza ikiwa imeshika nafasi ya 32 kati ya nchi 35 ambazo zimeweza kuambulia medali hadi, ambapo kuna takriban wanamichezo 5,054 wanashiriki katika Michezo hiyo kutoka nchi 72 na jumla ya Michezo 20 imechezwa.
Kenya ni ya 13 kimsimamo kwa kuwa na jumla ya medali 21 ikiwa ni 6 za dhahabu, 5 za Fedha na 10 za Shaba. Uganda ni ya 16 kwa kuwa na Medali 3 za Dhahabu na 2 za Shaba.
Australia yenye jumla ya medali 176, ambazo ni dhahahu 66, Fedha 57 na Shaba 53 ndio wanaoongoza, wakifuatiwa na wenyeji Uingereza ambao wana jumla ya medali 168 kiwa ni dhahabu 55, Fedha 60 na Shaba 53.
0 Comments