WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Innocent Bashungwa (kushoto) pamoja na mkewe Bi Jennifer Bashungwa (katikati) wakiwa kwenye mazungumzo na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Shree Goverdhannathji Haveli hapa nchini Bw Yogesh Manek (Kulia) walipohudhuria hafla ya ibada ya jamii hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Innocent Bashungwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla hiyo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Shree Goverdhannathji Haveli hapa nchini Bw Yogesh Manek akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Innocent Bashungwa (kulia) akizungumza na baadhi ya wageni waalikwa wakati wa hafla hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Abdulrahman Kinana (Kulia) akizungumza na baadhi ya wageni waalikwa wakati wa hafla hiyo
Hafla hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki ilihudhuliwa na wageni mbalimbali wakiwemo viongozi wa chama na serikali, mashirika na wawakilishi wa taasisi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
....................................................
Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Innocent Bashungwa amesema kuwa uhuru wa kuabudu pamoja na amani iliyopo nchini ni miongoni mwa sababu kubwa zinazovutia wawekazaji wengi kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza hapa nchini.
Waziri Bashungwa alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam, alipohudhulia hafla ya ibada ya jamii ya Wahindi wa dhehebu la Shree Goverdhannathji Haveli iliyofanyika mwishoni mwa wiki na kuhudhuliwa na wageni mbalimbali wakiwemo viongozi wa chama na serikali, mashirika na wawakilishi wa taasisi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Alisema kwa kutambua kwamba wawekezaji wengi wakubwa na wadogo wanatoka nje ya nchini na wamekua wakija na tamaduni pamoja na imani za dini tofauti, serikali imekuwa na jukumu muhimu la kuhakikisha inawapatia uhuru wa kuabudu sambamba na kuheshimu imani zao.
“Kutokana na hali hiyo wawekezaji wamekuwa wakija kwa wingi bila hofu ya kukosa uhuru wa kuabudu wala kuingiliwa kwa namna yoyote kwa kuwa hawaendi kinyume na sheria za nchi. Matokeo ya uwekezaji wao yamekuwa na tija kubwa kwa serikali Kuu pamoja na Halmashauri zetu kupitia kodi na ajira kwa wananchi waliopo kwenye maeneo ya uwekezaji,’’ alifafanua.
Alisema kwa upande wa serikali, kupitia viongozi mbalimbali imekuwa ikitumia vema matukio hayo kuhakikisha kwamba si tu inaonyesha ushirikiano na jamii hizo za kigeni bali pia kuwasilisha agenda mbalimbali za kiuchumi na maendeleo.
“Kwa kuwa matukio kama haya yamekuwa yakivutia si tu washiriki kutoka ndani ya nchi bali pia wapo washiriki wengi wanaotoka nje ya nchi wanaokuja kuungana na wenzao katika ibada kama hizi hivyo inakuwa rahisi kwetu pia kupenyeza agenda zetu kwao. Hivyo tunawashukuru na kuwapongeza wana jamii ya Shree Goverdhannathji Haveli hapa nchini kwa kutupatia heshima na fursa hii muhimu,’’ alisema Waziri Bashungwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Shree Goverdhannathji Haveli hapa nchini Bw Yogesh Manek aliishukuru serikali kwa namna inavyotoa uhuru wa jamii mbalimbali nchini kuabudu bila kuingiliwa sambamba na kuwatanguliza viongozi wa dini kwenye masuala mbalimbali ikiwemo maamuzi makubwa yanayohusu mustakabali wa taifa.
“Hii ni heshima kubwa na kupitia ushirikiano tunaoendelea kuupata kutoka serikalini na viongozi mmoja mmoja imekuwa rahisi pia hata kwa viongozi wa madhehebu na dini tofauti hapa nchini kushirikiana sisi kwa sisi kwenye matukio kama haya.’’
‘’Hii ni hatua nzuri zaidi si tu kidini bali pia kiuchumi kwa kuwa inaongeza mvuto hata kwa wale waliopo nje ya nchi kutamani kuja na kuwa sehemu ya wana jamii wa Tanzania na hivyo kuchochea uwekezaji,’’ alisema.
Bw Manek alibainisha kwamba mbali na masuala ya kiimani, jamii hiyo imekuwa mstari wa mbele pia kushirikiana na taasisi nyingine hapa nchini katika kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo ya miradi ya afya na elimu.
Tukio hilo la siku tatu limefanyika kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam likiwakutanisha pamoja watu kutoka jamii na taaluma tofauti ili kuonyesha talanta na upendo wao kwa Mungu wa jamii ya Wahindi anaefahamika kama Shree Krishna.
0 Comments