Ticker

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YAPIGA HATUA UTOAJI MIKOPO YA NYUMBA


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (katikati) akiwa kwenye Mkutano Mkuu wa 41 wa Taasisi ya Shelter Afrique unaofanyika katika mji wa Victoria Falls, Zimbabwe.

*******************

Na Munir Shemweta

Tanzania imepiga hatua katika utoaji mikopo ya nyumba ambapo jumla ya mikopo 6,182 imetolewa hadi sasa ikilinganishwa na mikopo 579 iliyotolewa kufikia mwaka 2009

Aidha, muda wa urejeshaji mikopo umeongezeka kutoka miaka 15 hadi 25 sambamba na riba ya mkopo kupungua kutoka asilimia 20 - 22 mwaka 2009 hadi asilimia 15-19 zinazotozwa sasa.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula tarehe 27 Julai 2022 katika Mkutano Mkuu wa 41 wa Taasisi ya Shelter Afrique unaoendelea kwenye Mji wa Victoria Falls nchini Zimbabwe ambapo Tanzania inahudhuria kama mwanachama wa Taasisisi hiyo.

Akichangia mada kuhusu jukumu la Benki Kuu kwenye soko la nyumba katika Bara la Afrika huku akitoa uzoefu wa Taasisi ya ‘Tanzania Mortage Refinance Company’ iliyoanzishwa kufuatia utekelezaji wa mradi wa mikopo ya nyumba uliokuwa ukisimamiwa na Benki Kuu, Dkt Mabula alisema kumekuwa na mafanikio makubwa toka kuanzishwa taasisi hiyo ambapo kwa sasa jumla ya Benki na Taasisi za fedha 33 zinatoa mikopo ya nyumba tofauti na ilivyokuwa kabla ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ambapo benki 3 tu ndizo zilizokuwa zikitoa mikopo.

‘’Kumekuwa na mafanikio makubwa toka kuanzishwa Taasisi ya Tanzania Mortage Refinance Company ambapo kwa sasa jumla ya benki na Taasisi za fedha 33 zinatoa mikopo ya nyumba tofauti na ilivyokuwa kabla ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ambapo benki 3 tu ndizo zilizokuwa zikitoa mikopo’’ alisema Dkt Mabula

Hata hivyo, Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwaeleza washiriki wa mkutano huo umuhimu wa Benki Kuu kusimamia ipasavyo Benki na Taasisi zinazotoa mikopo hiyo ili kuhakikisha zinatoa riba ambazo wananchi wataweza kumudu kwa kuwa nazo zinawezeshwa kupata mitaji nafuu.

Akielezea upungufu wa nyumba 3,000,000 na mahitaji ya nyumba 200,000 kwa kila mwaka nchini Tanzania, Dkt Mabula alisema, endapo benki na taasisi za fedha zitaendelea kuachiwa kutoza riba kubwa bila usimamizi haitafanikiwa kuwezesha wananchi hususan wa kipato cha chini kumudu gharama za nyumba bora.

‘’Endapo benki na taasisi za fedha zitaendelea kuachiwa kutoza riba kubwa bila usimamizi haitafanikiwa kuwezesha wananchi hususan wa kipato cha chini kumudu gharama za nyumba bora’’ alisema Dkt Mabula.

Mkutano Mkuu wa 41 wa Taasisi ya Shelter Afrique ulioanza Julai 25, 2022 unatarajiwa kumalizika kesho Julai 29, 2022 na unahudhuriwa na nchi wanachama wa Bara la Afrika ikiwemo Tanzania na umebeba kauli mbiu ya ‘Climate Change and the Built Environment’.

Post a Comment

0 Comments