*************************
Na. Majid Abdulkarim, WAF-RUKWA
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Mkirikiti amezindua kampeni ya chanjo kwa Wahudumu wa afya ngazi ya Jamii, watu mashuhuri na viongozi wa dini inayolenga kuongeza kasi ya uchanjaji wa chanjo dhidi ya Uviko-19 mkaoni humo.
Mhe. Mkirikiti amezindua kampeni hiyo leo Sumbawanga Mkoani Rukwa ambapo ametoa rai kwa Wataalamu wa afya kutoa ushirikiano wa karibu kwa Wahudumu wa afya ngazi ya Jamii, watu mashuhuri na viongozi wa dini ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa afua ya uchanjaji chanjo ya Uviko-19.
Akizungumza Mhe. Mkirikiti amesema uzinduzi kwa ngazi ya mikoa ulifanyika na chanjo ikaanza kutolewa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na asilimia 10.1 ya wana Rukwa wamekwisha chanja chanjo, ambayo ni idadi ndogo kulinganisha na mikoa mingine ya pembezoni kama Ruvuma (46%) na Katavi ((33%) hadi Julai 3 mwaka huu.
“Kwa Sababu hii siku ya leo tunafanya uzinduzi kwa kutumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuhamasisha ongezeko la watu wa mkoa huu kupata Chanjo ya Uviko-19”, ameeleza Mhe.Mkirikiti
Ameeleza kuwa uzoefu uliopatikana katika awamu hizi na mikakati ya utekelezaji wa kampeni umeonyesha kuwa kasi ya matumizi ya chanjo dhidi ya Uviko-19 huongezeka Zaidi wakati wa kampeni na mwenendo wa hali ya uchanjanji hushuka baada ya kampeni na kupelekea mikoa, hamlashauri na vituo kutofikia malengo ya kila siku yaliyowekwa.
Katika hatua nyingine Mhe. Mkirikiti ametoa rai kwa Wadau wote kushirikiana na Timu za Uendeshaji wa Huduma za Afya ngazi ya Mkoa na Halmashauri katika kuhakikisha afua ya uelimishaji wa kutambua umuhimu wa chanjo, namna inavyofanya kazi na faida zake kupitia huduma mkoba na tembezi kwa kushirikiana na wataalamu wa afya, wahamasishaji katika jamii (Wahudumu wa afya ngazi ya jamii), watu mashuhuri katika jamii, viongozi wa dini na viongozi wa mitaa
Pia ameongeza kuwa wananchi kwa kuwapa elimu na kuwapatia chanjo kwenye matukio mbalimbali ya matamasha, michezo, magulio na sherehe mbalimbali pamoja na kuwafuatulua walengwa wote ambao hawakupatiwa chanjo na kuhakikisha wananchi wote wa awali na wapya wanapata dozi ya pili ya chanjo
“Hakikisheni kuwa taarifa za wateja waliopata na wanaopata chanjo zinaingizwa katika mfumo wa chanjocovid system kwa wakati na ufanisi mzuri”, amesisitiza Mhe. Mkirikiti
Aidha,amekumbushia Waganga wakuu wa mikoa na halmashauri nchini kuhakikisha kuwa serikali na jamii katika mamlaka husika kama viongozi wa vitongoji,mitaa,Kijiji,kata,watu maarufu katika ngazi husika kama viongozi wa dini na viongozi wa kimila kushirikishwa kikamilifu wakati wa utejkelezaji wa afua za kuongeza kasi ya matumizi ya chanjo dhidi ya Uviko-19 wakati wote wa utekelezaji baada ya uzinduzi huu.
0 Comments