Ticker

6/recent/ticker-posts

NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI ZATAKIWA KUKUZA, KUENZI KISWAHILI

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

Nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimetakiwa kuweka mikakati ya muda mrefu ili kukuza, kuendeleza na kueneza lugha ya Kiswahili duniani.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Bw. Khamis Abdalla Saidi aliyemwakilisha Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe.Tabia Maulid Mwita katika Kongamano la kwanza la Siku ya Kiswahili Duniani lililoanza leo tarehe 6 Julai, 2022 Zanzibar.

Kongamano hilo linalongozwa na Kauli Mbiu: “Kiswahili kwa Amani, Ustawi na Utangamano wa Kikanda” litahitimishwa kwenye siku ya Kilele cha Siku ya Kiswahili duniani tarehe 7 Julai 2022.

Katika hotuba yake, Bw. Saidi amesema kuenea kwa Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki na Mataifa mengine ni bidhaa ya bishara, hivyo umuhimu wa Kiswahili ni mkubwa katika kupiga hatua ya kimaendeleo.

“Ni jukumu la kila mmoja wetu kukifuatilia Kiswahili katika kila hatua na kutafuta na kubuni njia na mikakati ya muda mrefu na ya kisasa ya kuikuza lugha hii adhimu ya Kiswahili,” amesema Bw. Saidi.

Bw. Saidi aliongeza Lugha ya Kiswahili inatakiwa itumike kama bidhaa inayouzwa na kupata tija. Kuna haja kubwa ya kuwekeza kuwasomesha wataalamu wa lugha kuwa na stadi na uwezo unaotakiwa katika kutoa huduma ya kufundisha, ukalimani, kutafrisi na kuandaa machapisho mbali mbali kwa Kiswahili.

“Ni jukumu la vyuo vikuu vya Afrika Mashariki kutilia mkazo mikakati ya muda mrefu ya uwekezaji wa kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa kufanya tafiti mbalimbali za lugha,” ameongeza Bw. Saidi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote amesema kuwa jumuiya ya Afrika Mashariki inapaswa kushirikiana kwa pamoja na wadau wa Lugha ya Kiswahili ili kuweza kupata uzoefu wa matumizi ya Kiswahili pamoja na kujadili changamoto za lugha hiyo ili kuimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili yataimarisha utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa lugha hii ni lugha ya biashara hivyo tunapaswa kujivunia lugha hii adhimu kwa maslahi mapana ya jumuiya yetu,” amesema Mhandisi Mlote.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (MS TCDC), Bi. Yusta Mganga amesema licha ya kuimarika kwa matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ukanda huo unapaswa kuchukua hatua madhubuti zaidi kwa ajili ya kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakuzwa na kuendelezwa miongoni mwa nchi ambazo bado hazijaimarika katika matumizi ya Kiswahili.

“Kuna njia mbalimbali za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili kama vile kufanya tafiti, uandaaji wa makongamano na semina mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya Kiswahili…….katika kuandhimisha siku hii muhimu ni vyema tukatafakari mafanikio ya Kiswahili katika ukanda wa Jumuiya yetu ili kuimarisha amani na utangamano wa kikanda,” amesema Bb. Mganga

Novemba 23, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) lilitangazwa rasmi kuwa tarehe 7 Julai ya kila mwaka ni siku maalumu ya kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani.

Februari 2022, Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika katika mkutano wake wa kawaida wa 35 walipitisha Kiswahili kama Lugha ya Kazi na mawasiliano mapana Barani Afrika.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, Bw. Khamis Abdalla Saidi akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani linalofanyika Zanzibar kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022


Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhandisi Steven Mlote akitoa hotuba yake katika Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar


Kaimu Katibu Mtendaji Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. James Jowi akizungumza na washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar


Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Dkt. Mwanahija Ali Juma akielezea mchango wa BAKIZA katika Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar


Meza Kuu wakifuatilia kikundi cha ngoma za asili kutoka Zanzibar wakati wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar


Washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani wakifuatilia kikundi cha ngoma za asili kutoka Zanzibar


Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota akitoa mchango wake katika Kongamano la Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar


Washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani wakiimba wimbo wa Taifa


Washiriki wa Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani wakifuatilia Kongamano hilo lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar


Meza Kuu katika picha ya pamoja na wawakilishi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Kongamano la siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika kuanzia tarehe 6 – 7 Julai, 2022 Zanzibar


Post a Comment

0 Comments