Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Itumbi, wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya baada ya kufika kijijini hapo kukagua kazi ya usambazaji umeme, kusikiliza kero za wananchi pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba akisalimiana na baadhi ya wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Itumbi, wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya baada ya kufika kijijini hapo kukagua kazi ya usambazaji umeme, kusikiliza kero za wananchi katika kijiji hicho pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
……………………………………
Imeelezwa kuwa, mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya kV 400 kutoka Iringa-Tanzania hadi nchini Zambia (TAZA) utaanza kutekelezwa Januari, 2023 na utakamilika Januari 2025 hali itakayopelekea kuimarika kwa upatikanaji umeme katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa pamoja kuiwezesha Tanzania kufanya biashara ya umeme katika nchi za kusini mwa Afrika na Afrika Mashariki.
Hayo yalielezwa wakati Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba alipofika katika eneo kutakapojengwa kituo cha kupoza na kukuza umeme cha Tunduma wilayani Momba, Mkoa wa Songwe ambapo kituo hicho ni moja kati ya vituo vitano vya kupoza umeme vitakavyojengwa kwenye mradi huo.
Mratibu wa Mradi wa TAZA, Mhandisi Elias Makunga alisema kuwa mradi huo utatekelezwa kwa jumla ya shilingi Trilioni 1.4 ambazo tayari Tanzania inazo na kwamba mradi utakuwa ni kiunganishi cha kwanza cha umeme wa juu kati ya Nchi Wanachama wa Kusini mwaka Afrika (SAPP) na Nchi Wanachama wa Mashariki mwa Afrika (EAPP) hali itakayochagiza biashara ya umeme kwani Tanzania itaweza kununua umeme nje ya nchi pale panapokuwa na upungufu na pia inaweza kuuza umeme nje ya nchi pale inapokuwa na ziada.
Aliongeza kuwa, shilingi Bilioni 23.1 zimetengwa kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi zaidi ya 6,198 waliopisha mradi huo ambapo Wizara ya fedha kuanzia mwezi wa Nane mwaka huu itafanya uhakiki ili kila mwananchi apate fidia stahiki kabla ya mradi kuanza kutekelezwa.
Waziri wa Nishati, January Makamba alisema kuwa mradi huo una muhimu wa kipekee kwani unaifanya Tanzania kuwa kiungo cha biashara ya umeme katika nchi za Kusini mwa Afrika na Mashariki mwa Afrika na pia mradi huo unaipa Tanzania nafasi ya kuendelea kuzalisha umeme zaidi hata utakaozidi mahitaji ya nchi kwani kuna fursa pia za biashara ya umeme.
“Tuna matumaini mradi utakamilika ndani ya miaka miwili kwani umetengwa katika vipande Nane hivyo kutakuwa na wakandarasi wengi watakaofanya kazi kwa kwa mpigo na hii itawezesha kujengwa kwa vituo vitano vya kupoza umeme pamoja na njia ya kusafirisha umeme kutoka Iringa hadi Rukwa pamoja na kipande cha kwenda mpaka wa Zambia.” Alisema Makamba
Aidha, katika kutekeleza kipaumbele cha Wizara ya Nishati cha kupeleka umeme kwenye maeneo ya uzalishaji ikiwepo migodi, Waziri wa Nishati alifika katika Kijiji cha Itumbi, wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya ili kuzungumza na wachimbaji wadogo ambapo aliwaeleza hatua zilizochukuliwa na Serikali za kupeleka umeme kwenye maeneo yao ya uchimbaji, kusikiliza kero zao pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Waziri wa Nishati aliwaeleza wachimbaji hao kuwa, maeneo 22 ya uchimbaji madini wilayani humo yatapata umeme kupitia mradi wa Gridi Mapato ambao tayari una shilingi bilioni 300 ambazo zitapeleka umeme kwenye maeneo ya uzalishaji ikiwemo migodi na viwanda nchini.
Aliongeza kuwa, wakandarasi wa kupeleka umeme kwenye migodi wilayani humo wataanza kazi mwezi wa 10 mwaka huu na kwamba kazi ya kusambaza umeme kwenye maeneo mengine ya kijiji hicho inaendelea baada ya kupata umeme takriban miezi mitatu iliyopita.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati ameendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia ambapo alitoa mitungi ya gesi kwa vikundi vya mamalishe ikiwa ni programu maalumu ya majaribio ambayo itawezesha Serikali kupata taarifa zitakazozewesha kutengeneza mpango mkubwa wa kitaifa wa usambazaji wa gesi nchini.
0 Comments