***********************
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
KIKUNDI cha ujasiliamali cha Shaurimoyo kilichopo kata ya Mzingani jijini Tanga, ambacho kinaundwa na watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (Waviu), wameipongeza halmashauri ya jiji la Tanga kwa kuonyesha utayari wa kusaidia kufanikisha shughuli zao za ujasiliamali, ikiwemo upendeleo katika upatikanaji wa mikopo pale watakapo kuwa tayari kuomba.
Pongezi na shukrani hizo wamezitoa mbele ya kamati ya Kudhibiti UKIMWI (CMAC) ya jiji la Tanga iliyowatembele kukagua miradi yao ya kiuchumi ya ufugaji wa kuku, utengenezaji wa sabuni za maji na batiki, na kuona mazingira ya ufanyaji kazi wa kikundi hicho.
Kamati ya kudhibiti UKIMWI chini ya Mwenyekiti wake, Naibu Meya wa jiji la Tanga, Colyvas Joseph ambaye pia ni diwani wa kata ya Maweni, leo imefanya ziara ya kutembelea shughuli na wadau wa UKIMWI ikiwa ni maandalizi ya vikao vya robo ya nne ya mwaka wa fedha 2021/2022.
Aidha kamati hiyo ilianza ziara yake kwa kutembelea kituo cha afya Makorora kuona utoaji wa huduma ya kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, na pia kupata taarifa ya uundaji wa vikundi vya wamama wanaoishi na virusi vya UKIMWI wanaohudhuria huduma hiyo.
Akitoa taarifa ya kitengo hicho, Mkuu wa Kitengo Ashura Mkindi amesema kitengo hicho huzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa kutoa elimu ya afya kwa mama mjamzito na mama anayenyonyesha wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
"Tunatoa kipimo cha DBS (Dried Blood Sample) kwa watoto waliozaliwa na mama mwenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI (HIV), kipimo hiki hufanyika pindi mtoto afikishapo umri wa wiki sita au siku 42 tangu kuzaliwa, hurudiwa tena mtoto afikishapo umri wa miezi tisa, mwaka mmoja na miezi mitatu, na mwaka mmoja na nusu, kipimo hiki hutumia SD Bioline" amefafanua Mkindi.
Lakini pia kamati hiyo imetembelea eneo la uwanja wa Saba Saba lililopo kata ya Nguvumali ikiwa ni moja ya eneo hatarishi kwa maambukizi ya UKIMWI, kutokana na shughuli zinazoendelea ndani ya uwanja huo.
Akitoa taarifa ya eneo hilo, Mratibu wa UKIMWI Jiji la Tanga Moses Kisibo amesema "uchunguzi uliofanyika katika eneo hilo umebainisha uwepo wa wingi wa wakina dada wanaojihusisha na biashara ya ngono, maarufu kama "changudoa" ambao wameweka maskani yao katika baa bubu na majengo mengine ndani ya uwanja huo".
Wajumbe wa Kamati waliweza kujionea mazingira ya eneo hilo na uhitaji wa hatua za makusudi katika kukabiliana na hali hiyo na kamati hiyo ilimalizia ziara yake kwa kutembelea Taasisi inayojihusisha na masuala ya vijana, kupinga ukatili wa kijinsia na kuibua vipaji vya vijana na kuwasaidia ili waweze kufikia malengo yao ya maisha - TAYOTA (Tanga Youth Talent Association).
Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Tree of Hope, chini ya ufadhili wa Botnar Fondation kupitia Mradi wa Tanga Yetu, wamepata ufadhili wa shillingi million 450 kwa ajili ya mradi wa kupiga vita aina zote za ukatili dhidi ya watoto na vijana balehe katika Jiji la Tanga.
Aidha mradi huo ni wa miezi sita na unatarajiwa kuwafikia watu elfu kumi ndani ya jiji la Tanga kuwapa elimu ya kupiga vita aina zote za ukatili, na tayari utekelezaji wake upo mwezi wa pili, ikisalia miezi minne ya kukamilika kwa mradi.
0 Comments