Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM inaweza kuwa Dubai ya Afrika na kuvutia biashara kubwa ya kimataifa iwapo Serikali itashirikiana na sekta binafsi kutatua tatizo sugu la ufanisi mdogo wa Bandari ya Dar es Salaam, linalochangiwa na utendaji finyu wa kampuni binafsi ya kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzania (TICTS), imebainika.
Ripoti mpya ya Bandari za Afrika Mashariki iliyotolewa na shirika la GBS Africa imesema kuwa ni lazima Bandari ya Dar es Salaam iongeze ufanisi kama inataka kushindana na bandari za Kenya, Afrika Kusini na Msumbiji.
TICTS, ambayo imekuwa inaendesha eneo la makontena la Bandari ya Dar es Salaam imetajwa kama kikwazo kikubwa kwa bandari hiyo kwa zaidi ya maka 20 kutokana na kushindwa kuongeza ufanisi na kukuza uchumi wa nchi.
Iwapo bandari ya Dar es Salaam itaongeza ufanisi, Tanzania itaweza kupunguza mfumuko wa bei, kwani waagizaji wa bidhaa huongeza bei za rejareja za bidhaa sokoni hapa nchini ili kufidia gharama kubwa inayotokana na ucheleweshaji wa upakuaji wa makontena kwenye eneo la TICTS.
“Bandari ya Dar es Salaam inahudumia zaidi ya asilimin 90 ya mzigo wa nchi,” ilisema ripoti hiyo ya GSA Africa.
“Ingawaje ni ndogo kuliko bandari za Duban (Afrika Kusini) na Maputo (Msumbiji), bandari ya Dar es Salaam inaikamata kwa kasi bandari ya Mombasa kwenye ushindani wa biashara ya mzigo unaopitia Bahari ya Hindi,” ilisema ripoti hiyo.
Kwa sasa, Bandari ya Dar es Salaam haijaweza kunufaika na changamoto za ufanisi wa Bandari ya Mombasa kwa kuvutia biashara zaidi kutoka nchi za ukanda huu wa Afrika ambazo hazina baharı, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Malawi, Uganda, Zambia, Rwanda, na Zimbabwe.
Wadau mbalimbali wanasema kuwa Bandari ya Dar es Salaam ingeweza kuzipiku Bandari za Kenya, Msumbiji na Afrika Kusini na kuwa kitovu cha kusafirisha mazao ya biashara na madani ya nchi za Afrika kama isingekuwa ni ufanisi duni wa upakuaji na ushushaji wa makontena.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwahi kutishia kuvunja mkataba wa TICTS kutokana na changamoto hizo za ufanisi.
Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza hadharani kuwa ufanisi duni wa Bandari ya Dar es Salaam hauwezi kuvumiliwa na Serikali yake ya Awamu ya 6 ambayo inafanya jitihada kubwa kuifungua nchi.
Rais Samia tayari amemtoa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari, Eric Hamissi, na kumteua Plasduce Mbossa kama bosi mpya wa kuongoza mageuzi ya Bandari nchini.
Sasa hivi serikali iko kwenye mazungumzo na kampuni ya TICTS kuhusu uwezekano wa kuwaongezea miaka mitano zaidi mkataba wao unapoisha mwezi Septemba mwaka huu.
Hata hivyo, wadau mbalimbali wamejitokeza kuishauri serikali kutoiongezea TICTS mkataba wake kutokana na kushindwa kuleta ufanisi unaotakiwa bandarini kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Chama cha ACT -Wazalendo kimeitaka Serikali kutoongeza mkataba na kampuni hiyo, huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Gabriel Migire, akinukuliwa akisema kuwa Serikali bado iko kwenye majadiliano na TICTS ili kuona kama iwaongezee mkataba au isiendelee.
“Timu yetu ya wataalamu iliyoundwa na Serikali bado ina muda wa kutosha wa kujadiliana na TICTS na hatimaye tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuamua kama tunaingia mkataba mwingine au hapana,” alisema Migire.
Hata hivyo, Msemaji wa sekta ya mawasiliano, teknolojia, habari na uchukuzi wa ACT Wazalendo, Ally Salehe, alisema suala la TICTS kukodishwa tena au la, linapaswa kuchukuliwa kwa umakini na kufikiwa uamuzi wenye kujali na kulinda uzalendo.
“Serikali isitishe nyongeza ya mkataba wa kukodisha kitengo cha makasha kati yake na TICTS, kwa kuwa ni wazi imeshindwa kukidhi matarajio ya Serikali yanayolenga kuongeza tija kwenye bandari yetu,” alisema Salehe.
Badala yake, ACT wameitaka Serikali kuiwezesha Mamlaka ya Bandari Tanzania kusimamia kitengo cha makasha kwenye Bandari ya Dar es Salaam katika wakati wa mpito, huku ikiendelea na mchakato wa kutafuta mwekezaji mwingine mwenye uwezo zaidi.
0 Comments