Ticker

6/recent/ticker-posts

BALOZI FATMA RAJAB AKUTANA NA UJUMBE WA SERIKALI YA OMAN

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab (kulia) akisalimiana na ujumbe wa Serikali ya Oman uliopomtembelea katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma. Ujumbe huo umeongozwa na Katibu Mkuu Wiazra ya Mambo ya Nje wa Oman, Mhe. Mohammed Bin Nasser Al Wahaibi.  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab (kulia) akizungumza na Katibu Mkuu Mambo ya Nje wa Oman, Mhe. Mohammed Bin Nasser Al Wahaibi leo tarehe 26 Julai 2022 katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab (wa pili kulia) na Katibu Mkuu Mambo ya Nje wa Oman, Mhe. Mohammed Bin Nasser Al Wahaibi (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania na Oman, baada ya kumaliza mazungumzo yao katika ofisi za Wizara jijini Dodoma tarehe 26 Julai 2022.

***********************

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amekutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Serikali ya Oman leo tarehe 26 Julai 2022 katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Oman kwakuwa nchi hizo zinashirikiana katika sekta za biashara, kilimo, uwekezaji, utalii, afya, elimu, ujenzi wa miundombinu,madini na uvuvi.

Ujumbe huo upo nchini kwa ziara ya siku 6 na unaongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje wa Oman, Mhe. Mohammed Bin Nasser Al Wahaibi ambaye ameambana na viongozi wengine wa Serikali ya Oman.

Pamoja na Balozi Fatma Rajab, ujumbe huo pia umefanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Antony Mtaka pamoja na uongozi wa jiji la Dodoma ambapo, ulipata wasaa wa kutembelea kiwanja kilichotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kujenga ofisi za Ubalozi wa Oman.

Aidha, tarehe 24 Julai 2022 ujumbe huo ulikutana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambapo ulifanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Ziara ya ujumbe huu ni matokeo ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Oman.

Post a Comment

0 Comments