Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MABULA AKUTANA NA MENEJA MKAZI WA KAMPUNI YA TEMBO NICKEL


Meneja Mkazi wa Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Ltd Benedict Busunzu akifafanua jambo kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula walipokutana jijini Dodoma Juni 15, 2022.


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula akizungumza na Meneja Mkazi wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Tembo Nickel Benedict Busunzu jijini Dodoma Juni 15, 2022. Kulia ni Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Tembo Nickel Corporation Ltd Sauda Simba.


Meneja Mkazi wa Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Benedict Busunzu (katikati) akifafanua jambo kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula walipokutana jijini Dodoma Juni 15, 2022. Kulia ni Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Tembo Nickel Corporation Ltd Sauda Simba. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)

………………………………..

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula amekutana na kufanya mazungumzo na Meneja Mkazi wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Nickel Tembo Nickel Corporation Ltd Benedict Busunzu.

Mapema mwaka 2021 Serikali ilitiliana saini mkataba na Kampuni ya LIZ Nickel ya Uingereza kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya Nickel Kabanga mkoani Kagera, pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuchenjulia madini mbalimbali kinachojengwa Kahama, Shinyanga.

Utiaji saini wa mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya LIZ Nickel kuliwezesha kuanzishwa kampuni ya pamoja inayoitwa Tembo Nickel Corporation Ltd ambayo ni kampuni ya ubia.

Akizungumza mkoani Dodoma Juni 14 2022, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Tembo Nickel Busunzu alimueleza Waziri wa Ardhi kuwa kampuni yake imejipanga vizuri kwa ajili ya kuanza mradi wa uchimbaji madini ya Nickel huko Kabanga, Ngara mkoani Kagera.

Alisema, hatua ya kwanza waliyochukua ni kuwaelimisha wananchi wanaoishi eneo la mradi ili kuwajengea ufahamu kwa lengo la kuepuka migogoro wakati wa ulipaji fidia kwa wale wananchi watakaohamishwa kupisha mradi.

‘’Tumetumia muda mrefu kuwaelimisha wananchi kabla ya kuanza uzalishaji wa Nickel hii itatusaidia kuepuka migogoro wakati wa zoezi la ulipaji fidia kwa wale wananchi watakaohamishwa kupisha mradi’’ alisema Busunzu.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alimueleza Meneja huyo mkazi wa Kampuni ya Tembo Nickel Corporation kuwa, uamuzi wa kutoa elimu kwa wananchi ni nzuri kwani utasaidia kuepuka migogoro hasa ile ya fidia kabla ya kuanza mradi.

‘’Hatua mliyochukua ya kutoa elimu mapema ni nzuri na itasadia kuondoa migogoro wakati wa zoezi la ulipaji fidia na ni vizuri pia mkafanya utaratibu wa kuthaminisha eneo lote la mradi kama ilivyofanyika kwenye mgodi wa Nyanzaga kule Sengerema’’ alisema Dkt Mabula.

Maoteo ya awali ya uzalishaji madini ya Nickel Kabanga wilayani Ngara mkoani Kagera utakuwa na wastani wa mauzo yenye thamani ya dola za marekani zaidi ya milioni 664 kwa mwaka.

Katika makubaliano ya mkataba wa Mradi huo Serikali itakuwa na umiliki usiopungua asilimia 16 ya hisa za mradi zisizolipiwa na zisizopungua thamani, hivyo kupata gawio kwenye faida zitakazopatikana baada ya kulipa kodi zote stahiki za serikali.

Utafiti uliofanywa na seriali ya Tanzania kuanzia mwsaka 1976 -1979 ulibaini kuwepo kwa madini ya Nickel katika mwamba unaoanzia eneo la Msongati nchini Burundi hadi Kabanga ambapo kiasi kikubwa cha Nickel kinapatikana Kabanga ni ya daraja la kwanza.

Post a Comment

0 Comments