Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Bi. Catherine Bamwenzaki akifungua Warsha ya Mafunzo ya kuwajengea uelewa wadau kuhusu mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Nationally Determined Contribution – NDC). Warsha hiyo ya siku nne inafanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) na kuwashirikisha wataalamu kutoka Wizara za Kisekta, Taasisi za Elimu na Tafiti, Asasi za Kiraia na Sekta binafsi.
Washiriki wa Warsha ya Mafunzo ya kujenga uelewa wadau kuhusu mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Nationally Determined Contribution – NDC) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa warsha hiyo leo tarehe 22/06/2022 katika Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA). Sehemu ya wataalamu wa Mazingira kutoka Mikoa mbalimbali wakiwa katika vikundi baada ya kupata mafunzo ya mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Nationally Determined Contribution – NDC). Mafunzo hayo yanafanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine – SUA na kutolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
************
Ofisi ya Makamu wa Rais imekutana na Maafisa Mazingira kutoka Mikoa yote nchini kwa lengo la kujadili mchango wa Taifa wa Kukabiliana na mabadiliko tabianchi (NDC). Mkurugenzi Msadizi Idara ya Mazingira Bi. Catherine Bamwenzaki amesema warsha hiyo itakua ya siku nne na itajumuisha wadau mbalimbali. Bi. Catherine ametaja baadhi ya wadau hao wanaokutana kujadili mchango huo wa Taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi kuwa ni pamoja na sekta binafsi, Maafisa mazingira kutoka mikoa yote pamoja waandishi wa habari. Anasema kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kila Nchi inatakiwa kuonesha mkakati wa jinsi ya kupambana na Mabadiliko tabianchi kwa kupunguza uzalishaji wa gesi joto. Kwa upande wake Afisa Mazingira kutoka Mkoa Geita Bw. Tito Mlelwa amesema changamoto ya mabadiliko tabianchi ni suala la kidunia kwa ujumla hivyo warsha hiyo itampa fursa ya kuona mbinu za Kukabiliana na changamoto hiyo kimkakati. Mlelwa anasema Mkoa wa Geita unakabiliwa na ukame maeneo mengi ambayo chanzo chake Ni uharibifu wa Mazingira. Naye Mratibu wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini - EBARR, Dkt. Makuru Nyarobi amesema mradi huo unajikita katika kuwajengea uwezo wananchi hasa vijijini kutumia nyezo na vifaa visivyoleta uchafuzi Mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kuhakikisha malambo yanachimbwa kwa Wafugaji ili iwe rahisi kuwa na upatikanaji wa maji pamoja na kutoa mizinga ya nyuki. Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) na ni miongoni mwa nchi zilizowasilisha Mchango wake wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Nationally Determined Contribution (NDC) kwenye Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, tarehe 30 Julai 2021. Licha ya kuwasilisha NDC katika Sekretariet, elimu kwa wadau hususan jamii zinazoathirika na mabadiliko ya tabianchi pamoja fursa za kukabiliana na athari zilizobainishwa ni jambo la muhimu sana. Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na UNDP wameandaa warsha katika Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) ili kuendelea kujenga uelewa kuhusu NDC na fursa zake. Warsha inafanyika katika ukumbi wa Institute of Continuing Studies, Morogoro.
0 Comments