*******************************
Na.WAF-Dar es Salaam
Wadau wa Mfuko wa Afya wa pamoja nchini (Health Basket Fund) wamepanga kuchangia kiasi cha shilingi Bilioni 98.1 kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini kwa mwaka 2022/2023.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kikao cha kujadili uboreshaji wa mfuko huo kupitia ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali na wadau Jijini Dar Es Salaam.
“Kwa niaba ya Serikali tunawashukuru wadau wetu wanaochangia kwa pamoja kwenye Mfuko wa Afya na tunatarajia kwa Mwaka wa fedha ujao wa 2022/23 wadau wetu kwa pamoja kuchangia Shilingi Bilioni 98.1 na fedha hizo zitaingizwa moja kwa moja kwenye akaunti za Vituo vya kutolea huduma za Afya nchini” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amesema katika mwaka wa fedha uliopita wadau kupitia Mfuko walichangia kiasi cha shilingi bilioni 74.3 ambapo asilimia 90 ya fedha zimekwenda kwenye Halmashauri na zimeingizwa moja kwa moja kwenye Zahanati, Vituo vya Afya pamoja na Hospitali za Wilaya nchini.
Aidha, Waziri Ummy Mwalimu amesema upo umuhimu kwa wadau wa maendeleo kuchanga fedha kwa pamoja na kuweka kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja na kusema kuwa kufanya hivyo ni kuzingatia Mifumo na taratibu za Serikali za kutoa fedha kwa ajili ya Huduma za Afya nchini pamoja na kuwekeza fedha kwenye maeneo ya vipaumbele vya Serikali.
“Fedha zinazoingizwa nchini kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za afya tunapenda ziingizwe kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja ili tuweke kushirikiana kufanya kazi pamoja na kupata matokea ya haraka kwa pamoja, mapendekezo yetu wadau wengine wachangia kupitia mfuko huo kwani tumeona mafanikio makubwa" amefafanua Waziri Ummy Mwalimu.
Kwa upande wake Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange ameshukuru wadau hao kwa kuendela kutoa ushirikiano na Serikali na kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Mhe. Dugange amepongeza wadau hao kwa kuongeza kiwango cha fedha kutoka Shilingi Bilioni 74.3 mwaka wa fedha 2021/22 hadi Bilioni 98.1 kwa mwaka wa fedha 2022/23 na kusema kuwa kupitia mchango huo pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanyika, Serikali kufanya mapinduzi makubwa kwenye ubora wa huduma za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Mhe. Dugange amesema kuwa asilimia 33.3 ya fedha hizo hutumika kwenda kununua dawa, vifaatiba na ‘reagents’ kwa ajili ya vipimo vya maabara ikiwa na pamoja kuboresha huduma za mama na mtoto katika vituo vya kutolea huduma za afya.
“Kwa mwaka huu wa fedha 2022/23 vituo zaidi ya 175 vimepata vifaatiba kwa ajili ya huduma za upasuaji, lakini kwa mwaka ujao wa fedha, tunatarajia vituo zaidi ya 225 vitapata vifaatiba” amefafanua Mhe. Dugange
Akizungumza kwa niaba ya Wadau wanaochangia katika Mfuko wa Afya wa pamoja, akizungumza na vyombo vya Habari Dkt. Peter Nyela Meneja wa Program ya Afya kutoka Ubalozi wa ‘Ireland’ wanafanya hivyo kusaidia Serikali ili kuhakikisha Vituo vya kutolea huduma za afya nchini vinakuwa na dawa, kurahisisha huduma nyinginezo ikiwemo huduma za rufaa, pamoja na motisha kwa watoa huduma za afya nchini.
"Huu ni ushirikiano mzuri sana baina ya Serikali na Wadau wa Maendeleo kuweza kufanya kazi kwa pamoja kuweza kusaidia kuboresha huduma za Afya nchini, Sisi kama Wadau kwa pamoja tutaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha Sekta ya Afya nchini” amefafanua Dkt. Nyela.
Mfuko wa Afya wa Pamoja umedumu kwa miaka 23 hadi kufikia leo ambapo ni muunganiko wa pamoja baina ya Serikali na Wadau wa Maendeleo kutoka Denmark, Korea, Ireland, Switzerland, Canada, UNFPA, UNCEF na Benki ya Dunia ambao huchangia katika huduma za afya nchini kwa kutoa fedha na kuziweka kwenye akaunti moja na fedha hizo kutolewa moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
0 Comments