Ticker

6/recent/ticker-posts

UVCCM SHINYANGA WATOA MAAZIMIO KWA RAIS SAMIA



Na Mwandishi Wetu

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (ALAT) Mhe. Sima Costantine Sima amewahamasisha vijana wa Chama Cha Mapinduzi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zinazoendelea ndani ya chama ili kuendelea kuimarisha umoja wa vijana nchini.

Akizungumza wakati akifungua Kikao cha baraza la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Shinyanga kilichofanyika Juni 29,2022 Sima amesema vijana wana nafasi kubwa ya kugombea nafasi za uongozi huku akiwataka kusimama imara katika kukilinda chama na viongozi wake.

Sima ambaye ni Mstahiki Meya wa jiji la Mwanza amewakumbusha madiwani wote kuendelea kuwa mabalozi wazuri katika kuendelea kulinda kundi la vijana ili waweze kufikia ndoto zao katika umoja wao kupitia chama hicho cha CCM.

”Vijana wengi tumekuwa tukikatishwa tamaa, zinapofika nyakati za uchaguzi kila kijana anayo nafasi ya kufika sehemu yoyote anayotamani kufika, najua wengi tunatembea na ndoto zetu ukitaka kufika mbali lazima ndoto yako uipitishe ,ukitaka kufanikiwa lazima ndoto yako iwe kubwa zaidi vijana katika kipindi hiki ambacho tunaenda kwenye uchaguzi shauku yangu kubwa ni kuona kijana yeyote wa Shinyanga akajaribu nafasi ambayo kesho atakuja kuiona nafasi yenye manufaa kwake”, amesema Sima.

Sima ameahidi kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili katika UVCCM Mkoa wa Shinyanga ikiwemo changamoto ya ukosefu wa baadhi ya vifaa katika ujenzi wa nyumba za viongozi wa umoja huo.

Akizungumzia kuhusu maazimio ya Baraza Kuu la UVCCM mkoa wa Shinyanga, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Shinyanga Baraka Shemahonge amesema Vijana wa CCM Mkoa wa Shinyanga wanampongeza Mhe. Rais kwa kuendelea kutoa ajira mbalimbali katika kada mbalimbali.

"Tunashukuru sana Mhe. Rais Samia kwa jitihada anazoendelea nazo kuhakikisha kila Mtanzania anapata ajira iwe ya Serikali ama Sekta Binafsi. Pia tunampongeza Mhe. Rais kwa maono yake makubwa katika miundombinu ya Elimu, ameleta Shilingi Bilioni 6 wa ajili ya Ujenzi wa Shule maalum ya wasichana inayojengwa katika Manispaa ya Shinyanga. Lakini pia ameleta fedha za kujenga shule za Sekondari katika kila kata ambayo haikuwa na shule ya Sekondari", amesema Shemahonge.

"Tunamshukuru Mhe. Rais Samia katika Sekta ya Maji ambapo Tshs. 195 Bilioni zimetolewa na Serikali ya awamu ya sita katika kuongoza mtandao wa Maji katika Manispaa ya Shinyanga na Halmashauri ya Shinyanga DC. Katika Sekta ya Afya Serikali ya awamu ya sita imetenga na kuanza kujenga vituo vya afya katika tarafa zote ambao hazikuwa na vituo vya afya",ameongeza Shemahonge.

Aidha amesema wanampongeza na kumshukuru Rais Samia kwa namna ambavyo anapambana yeye na wasaidizi wake kuhakikisha wananchi wanapata unafuu wa mfumko wa bei za mafuta, juhudi hizi za kutenga Shilingi Bilioni 100 kila mwezi ni mahsusi na muhimu katika kuwasaidia wananchi katika mfumko wa bei unaotokana na madhara ya vita za Urusi na Ukraine.

"Tunampongeza Mhe. Rais Samia na Serikali yake katika maandalizi mazuri kuelekea Sensa ya watu na Makazi mnamo tarehe 23/08/2022. Elimu na hamasa kubwa imetolewa inatolewa na Serikali kwa wananchi juu ya umuhimu wa Sensa ya watu na Makazi 2022",amesema Shemahonge.

"Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuondoa ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita. Huu ni unafuu mkubwa kwa wazazi na walezi",ameongeza.

Shemahonge amewahamasisha vijana katika Mkoa wa Shinyanga kuchukua fomu za kugombea nafasi ya uongozi bila kusita kwa kuzingatia misingi na utaratibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Awali akisoma taarifa fupi ya utekelezaji Katibu wa UVCCM Mkoa wa Shinyanga Raphael Nyandi ameeleza baadhi ya mafanikio katika jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza wananchama wapya wa umoja wa vijana kutoka Chama Cha Mapinduzi.

”Tumefanya ziara kuangalia uhai wa jumuiya na utekelezaji wa ilani hasa maeneo ambayo yanahitaji utoaji wa mikopo kwa vijana tumefanikiwa kuingiza wanachama wapya wa umoja wa wa vijana kutoka chama cha mapinduzi kwa wingi kutoka mashuleni, vyuo na kwenye maeneo mbalimbali na mashina ya wakeleketwa tumefanikiwa kujenga nyumba ya watumishi wa umoja wa vijana Mkoa na Wilaya zote za Mkoa wa Shinyanga”, amesema.

Nyandi ametaja baadhi ya changamoto zinazowakabili kwenye jumuiya hiyo ikiwemo changamoto ya ukosefu wa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba za viongozi.

”Lakini pamoja na mafanikio hayo makubwa tunazo changamoto kwanza ukosefu wa fedha kwa ajili ya kukamilisha majengo ya watendaji kutokana na viongozi”, amesema Nyandi.
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (ALAT) Mhe. Sima Costantine Sima akifungua Kikao cha baraza la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Shinyanga kilichofanyika Juni 29,2022
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Shinyanga Baraka Shemahonge akizungumza kwenye Kikao cha baraza la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Shinyanga kilichofanyika Juni 29,2022
Katibu wa UVCCM Mkoa wa Shinyanga Raphael Nyandi akizungumza kwenye Kikao cha baraza la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Shinyanga kilichofanyika Juni 29,2022


Post a Comment

0 Comments