*******************************
Kituo cha Uwekezaji Tanzania kinaendelea na maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutoa elimu ya Uwekezaji kwa wananchi na wawekezaji kwa ujumla.
Kauli mbiu inayoongoza wiki hii ni “Nafasi ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda katika masuala mapya yanayojitokeza kuhusu utoaji wa huduma na urejeshaji wakati na baada ya Janga la Corona”
Akizungumza na vyombo vya habari Kaimu Mkurugenzi Huduma kwa Wawekezaji Bi. Anna Lyimo akimuwakilisha Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) amewakaribisha wananchi na wawekezaji kutembelea ofisi za TIC ili kupata elimu juu ya fursa mbalimbali za Uwekezaji pamoja na tafiti mbalimbali zinazoibua fursa za Uwekezaji nchini.
Bi. Lyimo amesema, “Tangu tarehe 16 Juni, 2022 tumekuwa na maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma itakayoadhimishwa mpaka tarehe 23 Juni na kilele chake tarehe 24 Juni 2022 na Kituo katika uwajibikaji katika maswala ya kijamii kitatembelea hospitali ya Ocean Road.
Aidha Bi. Lyimo amesisitiza kuwa, “Wiki ya Utumishi wa Umma inawapa fursa wafanyanyakazi waliopo pembezoni kutoa mapendekezo na changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao”
“Kituo kimedhamiria kuelimisha juu ya maboresho ya teknolojia katika utoaji wa huduma chini ya Kituo cha Mahala Pamoja namna kinavyorahisisha upatikanaji wa leseni, vibali, na usajili wa mradi”, ameongeza Bi. Lyimo.
Wageni waliotembelea TIC wamefurahishwa sana na elimu ya Uwekezaji waliyoipata katika ofisi za TIC na Bwana Venkatesh Rokkam kutoka Kampuni ya Blue Sky ametembelea TIC ili kufahamu hatua za kupata cheti cha Uwekezaji ili nae awe mwanafamilia ya TIC.
“Kampuni yetu inapenda kuwa mwanafamilia wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, hivyo nimefika hapa ili kupata maelezo ya namna ya kupata cheti cha Uwekezaji lakini pia kupata elimu juu ya fursa nyingine za uwekezaji zilizopo hapa nchini” amesema Bw. Rokkam
Ameishukuru timu nzima ya TIC kwa elimu inayotoa juu ya uwekezaji na ameahidi kumleta Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Blue Sky ambae ni raia wa nchini India ili na yeye apate elimu hii ya uwekezaji na kuzifahamu fursa za uwekezaji zilizopo nchini.
Bwana Godwin Swai Mshauri wa kujitegemea(consultant) kutoka kampuni ya Vision Promotors amesema amekifahamu Kituo cha Uwekezaji takribani miaka 15 iliyopita na amekuwa akishirikiana nacho kwa karibu sana kwa kuleta wawekezaji.
“Zaidi ya asilimia 96 ya wawekezaji niliowaleta TIC wamefanikiwa kuwekeza nchini na mradi ambao mpaka sasa unafanya vizuri ni mradi wa majengo ya DEMO yaliyopo Makumbusho jijini Dar es Salaam nw Multichoise Safaris, Arusha na miradi mingine mingi” amesema Bw. Swai.
Katika maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma wageni zaidi ya 50 wameweza kupata elimu juu ya fursa za uwekezaji na namna mbalimbali za huduma zinazotolewa na Kituo cha Uwekezaji hasa kupitia Kituo cha Mahala Pamoja ( One Stop Facilitation Centre).
TIC inawakaribisha wananchi wote pamoja na wadau wa uwekezaji kutembelea ofisi za TIC makao makuu jijini Dar es Salaam zilizopo Mtaa wa Shaaban Robert.
0 Comments