Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUONGEZA UPATIKANAJI WA MAJISAFI KWA KUTUMIA VYANZO VYA MITO NA MAZIWA

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akisaini kitabu cha wageni ofisini kwa Mkuu wa Mkoa Katavi. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akizungumza wakati wa ziara yake Mkoani Katavi. Kulia ni Katibu Tawala Mkoa wa Katavi, Rodrick Mpogolo.

Meneja RUWASA Mkoa wa Katavi, Mhandisi Peter Ngunula (kulia) akizungumza wakati wa ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (hayupo pichani) Mkoani Katavi.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (katikati) akielekeza jambo alipotembelea eneo la Ziwa Tanganyika katika Kata ya Karema Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi. Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga alipotembelea eneo la Ziwa Tanganyika katika Kata ya Karema Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi.

***************************

Na Mohamed Saif, Katavi

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema Serikali imedhamiria kutumia vyanzo vya maji vya Mito na Maziwa ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo yaliyo jirani na vyanzo hivyo.

Ametoa kauli hiyo Mkoani Katavi Juni 23, 2022 alipowasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kutambulisha ziara yake mkoani humo.

Mhandisi Sanga amesema Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameielekeza Wizara kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wote kwa kutumia vyanzo vya maji vya uhakika ikiwemo mito na maziwa makuu.

"Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza wananchi wote wafikishiwe huduma ya maji nasi Wizara tunatekeleza kwa kuhakikisha huduma inafika kwa wananchi," alisema Mhandisi Sanga.

Alibainisha kuwa ziara yake Mkoani humo inafuatia maelekezo ya Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) baada ya kufanya ziara mkoani humo na kujionea hali ya upatikanaji wa maji.

"Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara mkoani hapa alielekeza chanzo toshelevu ni Ziwa Tanganyika na kupitia ziara yangu nitatembelea eneo hilo la ziwa na miradi mingine ya maji mkoani hapa kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji," alisema Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga alibainisha mikakati thabiti ya Wizara ya Maji katika kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya maji maeneo mbalimbali nchini mojawapo ikiwa ni hiyo ya kutumia vyanzo toshelevu vya maji.

"Tumedhamiria mikoa yote yenye vyanzo toshelevu tuvitumie ipasavyo, mmeshuhudia hivi karibuni Mhe. Rais alituzindulia mradi wa kwanza katika historia ya nchi yetu kutumia chanzo cha Mto Kagera," alibainisha Katibu Mkuu Sanga.

Alisema mafaniko makubwa yameonekana katika kutumia vyanzo hivyo vikubwa akitolea mfano chanzo cha Ziwa Victoria ambacho kimekuwa msaada mkubwa kwa mikoa mingi jirani yaani Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera, Shinyanga na Tabora na lengo ni kutanua zaidi hadi Dodoma.

Mhandisi Sanga vilevile alielezea matumizi ya Ziwa Tanganyika ambapo alisema Mkoa wa Kigoma umekwishaanza kunufaika na kwamba hatua inayofuatia ni kutumia chanzo hicho kunufaisha maeneo mengine kama inavyofanyika kwenye Ziwa Victoria.

"Ziwa Tanganyika ni chanzo sahihi kwa Mkoa wa Katavi nao kunufaika na huduma toshelevu ya majisafi na salama; ni ziwa lenye kina kirefu na pia halina athari za uchafuzi," alisema Katibu Mkuu Sanga.

Katibu Mkuu Sanga yupo Mkoani Katavi kwa ziara ya siku mbili ya kukagua miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa mkoani humo sambamba na kutembelea eneo la chanzo cha maji Ziwa Tanganyika na baadaye kuzungumza na wafanyakazi.

Post a Comment

0 Comments