************************
Na Mwandishi wa NCAA, Ngorongoro Kreta Arusha.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi NCAA, Dkt. Christopher Timbuka leo tarehe 11 Juni, 2022 amepokea ugeni wa wataalam wa Uhifadhi kutoka Kenya Wildlife Service (KWS) ambao walitembelea Ngorongoro Kreta kwa lengo la kuangalia maandalizi ya kupokea faru weusi watano (5) wanaotarajiwa kuletwa nchini muda wowote kuanzia sasa.
Dk.Timbuka ameuelezea kuwa ujumbe huo kuwa, NCAA ipo tayari kupokea faru hao kwa kuwa shughuli za ulinzi na mazingira ya uhifadhi wa Faru yameendelea kuimarishwa katika hifadhi ya Ngorongoro.
“Hadi sasa jitihada mbalimbali zimechukuliwa katika kuhifadhi faru na zimeleta matokeo chanya na kupelekea idadi ya faru ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kuzidi kuongezeka, na sasa tumeshandaa mazingira na utayari wa kupokea faru wengine watano kutoka Nchini Kenya.” Aliongeza Dkt. Timbuka.
Amebainisha kuwa idadi ya Faru hao watano wataletwa Tanzania kwa awamu mbili; ambapo awamu ya kwanza itahusisha Faru watatu (3) na awamu ya pili itahusisha faru wawili (2).
Akitoa wasilisho maalum kuhusu uhifadhi wa faru ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Mratibu wa Kitengo cha Faru NCAA Bw. Deogratius Maige alieleza ujumbe huo kuwa NCAA inatumia njia mbalimbali za teknolojia ya kisasa ili kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa mnyama Faru ambayo imeleta matunda katika kuongeza idadi na kuwalinda faru hao.
Wataalum kutoka Kenya wamekuja kutembelea eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ili kujiridhisha na maandalizi yanayofanyika kuwapokea faru hao ambapo wametembelea Bonde la Ngorongoro na kukugua boma la faru linaloandaliwa kwa ajili ya kupokea faru hao na maeneo ambayo wataishi baada ya kuachiliwa kutoka kwenye boma pamoja na kuona Faru wanavyoishi katika mazingira yao ya asili.
Ujumbe wa huo uliohusisha wataalam kutoka Kenya uliongozwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mafunzo na Utafiti wa wanyamapori Kenya Dkt. Patrick Omondi, na timu ya wataalam wa masuala ya Uhifadhi kutoka Tanzania iliongozwa na Mratibu wa Faru Taifa Bw. Philbert Ngoti. Wataalam wote hawa kutoka Tanzania na Kenya, ni sehemu ya Kamati ya pamoja ya Ufundi.
Ikumbukwe kuwa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni moja ya maeneo ya Uhifadhi ambayo faru weusi huonekana kwa urahisi katika mazingira yake ya asili sambamba na na kuwa na rekodi ya Faru mweusi mwenye umri mkubwa duniani aliyefahamika kwa jina la Faru Fausta, aliyeishi miaka 57 katika hifadhi ya Ngorongoro.
0 Comments