Ticker

6/recent/ticker-posts

MZEE MAARUFU 'MARIA NTOWE' , MCHIMBAJI MADINI ANAYEHAMASISHA WANAWAKE KUKAMATA FURSA ZA KIUCHUMI


Mzee Maarufu Bi. Maria Stephen Ntowe (70) akielezea namna alivyotumia fursa ya uchimbaji madini kujipatia kipato na kujiinua kiuchumi baada ya kupewa mafunzo ya kujiamini na kuchukua fursa za kazi zinazofanywa na wanaume kwani na wanawake wanaweza kuzifanya kwenye kikao cha mrejesho wa Wasaidizi wa Kisheria na Vituo vya Taarifa na Maarifa kata ya Lunguya na Shilela halmashauri ya Msalala mkoani Shinyangakwa kuhusu masuala ya Kisheria na kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye maeneo yao kilichoandaliwa na TGNP kupitia UNFPA kwa ufadhili wa KOICA. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mzee Maarufu Bi. Maria Stephen Ntowe (70) akielezea namna alivyotumia fursa ya uchimbaji madini kujipatia kipato na kujiinua kiuchumi.
Mzee Maarufu Bi. Maria Stephen Ntowe (70) akielezea mafanikio yaliyofikiwa katika jamii ambapo sasa wanawake wanashiriki shughuli za uchimbaji madini kwenye kikao cha mrejesho wa Wasaidizi wa Kisheria na Vituo vya Taarifa na Maarifa kata ya Lunguya na Shilela halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga kuhusu masuala ya Kisheria na kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye maeneo yao kilichoandaliwa na TGNP kupitia UNFPA kwa ufadhili wa KOICA.
Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Msaada wa Kisheria mkoa wa Shinyanga, John Shija ambaye ni Mratibu wa shughuli zinazofanywa na TGNP Mkoa wa Shinyanga akizungumza kwenye kikao cha mrejesho wa Wasaidizi wa Kisheria na Vituo vya Taarifa na Maarifa kata ya Lunguya na Shilela halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga kuhusu masuala ya Kisheria na kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye maeneo yao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Msaada wa Kisheria mkoa wa Shinyanga, John Shija ambaye ni Mratibu wa shughuli zinazofanywa na TGNP Mkoa wa Shinyanga akizungumza kwenye kikao cha mrejesho wa Wasaidizi wa Kisheria na Vituo vya Taarifa na Maarifa kata ya Lunguya na Shilela halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga kuhusu masuala ya Kisheria na kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye maeneo yao.


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mzee Maarufu Bi. Maria Stephen Ntowe (70) mkazi wa kijiji cha Lunguya kata ya Lunguya Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga amewataka wanawake kuchangamkia fursa ya uchimbaji madini ili waweze kujipatia kipato na kujiinua kiuchumi kwani sasa ile ya mila potofu kuwa Wanawake wakiingia katika migodi wanaleta mikosi imepotea hivyo shughuli za uchimbaji madini zinafanywa na wanaume na wanawake.


Bi. Maria ametoa rai hiyo Jumamosi Juni 4,2022 kwenye kikao cha mrejesho wa Wasaidizi wa Kisheria na Vituo vya Taarifa na Maarifa kata ya Lunguya na Shilela halmashauri ya Msalala mkoani Shinyangakwa kuhusu masuala ya Kisheria na kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia katika jamii ikiwa ni mwendelezo wa kazi ya Mradi wa Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wananchi kiuchumi Mkoa wa Shinyanga katika halmashauri ya Msalala unaotekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia Shirika la Kimataifa la UNFPA kwa ufadhili wa KOICA.


Bi. Maria ambaye pia ni Mhasibu wa Wazee Halmashauri ya Msalala amesema kazi ya kuchimba madini ni kazi ya jinsi zote hivyo wanawake na wanawake wanayo nafasi ya kushirikiana na wanaume kuchimba madini.


"Zamani tulikuwa tunaambiwa kuwa wanawake tuna mikosi kama mti uitwao 'Mzima' kwamba tukiingia mgodini dhahabu inakimbia .Mti wa Mzima hauruhusiwi kuonekana mgodini kwa sabab unaaminika kuzima bahati hivyo wanawake tulifananishwa na mti huo kwamba ni mkosi kuonekana mgodini lakini sasa mambo yamebadilika hizo mila na imani potofu zimepungua wanawake wengi sasa wanashiriki shughuli za uchimbaji madini",ameeleza Bi. Maria.


ALIANZAJE SHUGHULI ZA UCHIMBAJI MADINI


Bi. Maria anasema alipata hamasa ya kuanza shughuli za uchimbaji madini baada ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kuanza kutekeleza shughuli zake katika kata ya Lunguya na Shilela halmashauri ya Msalala Oktoba 2020 ambapo TGNP ilikutana na wanawake na kuwapa mafunzo jinsi ya kujiamini na kuchukua fursa za kazi zinazofanywa na wanaume kwamba hata wanawake wanaweza kuzifanya.


"Mwanzo niliona ni kama ndoto wanawake kuwa wachimbaji baada ya kupata mafunzo ya TGNP nilipata ujasiri na kujiamini kuwa naweza kufanya kazi zinazofanywa na wanaume, nikaona fursa ya kiuchumi na nilivutiwa na wanawake ambao tayari walikuwa wameanza shughuli za uchimbaji na sasa naendelea kunufaika na kazi hii. Na sasa naamini kuwa wanawake tunaweza kumiliki rasilimali zetu na zikatusaidia kujiinua kiuchumi", amesema Bi. Maria.


Bi. Maria ambaye ni mkazi wa Lunguya anayemiliki duara tatu katika mgodi wa dhahabu wa Nyamishiga kata ya Lunguya anasema alianza shughuli za uchimbaji madini mwaka 2020 kwenye shamba lake na kuanza kumiliki duara katika mgodi huo mwezi Januari 2022 alipojiunga na kikundi cha wachimbaji.


"Kuwa mchimbaji wa madini siyo lazima uwe unachimba mwenyewe bali unaweza kujiunga katika kikundi na badala ya kuchimba unatoa pesa kama mimi ninavyofanya, ukitoa fedha unakuwa mwanachama wa kikundi, nina maduara yangu matatu wanachimba wengine lakini mali inayopatikana nanufaika nayo", amesema Bi. Maria.


Mzee huyo maarufu amesema pia anatumikia Idara ya Felo (mawe ya dhahabu yenye hali ya chini) ambapo majukumu yake ni kuweka nembo kwenye mifuko inayobeba mawe hayo.


Amewahamasisha wanawake kujiamini na kuchangamkia fursa za uchumi zilizopo kwenye maeneo yao ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia unaosababishwa na hali duni ya kiuchumi katika kaya.

Post a Comment

0 Comments