Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima akiongea na wajumbe katika kikao cha Bodi ya Barabara mkoani humo.
**************************
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
WAJUMBE wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Tanga wameziomba Wakala zinazohusika na barabara TANROADS na TARURA kuondoa rasta barabarani na kurekebisha matuta sehemu ambazo hazina ulazima.
Wakizungumza kwenye kikao cha Bodi ya Barabara juzi wajumbe hao walisema kuna rasta ambazo zimewekwa kwenye maeneo ambayo siyo rafiki na zinaleta madhara kwa watumiaji wa barabara hizo jambo ambalo kwa sasa wenye magari hawazitumii.
"Kuanzia Segera hadi hapa Tanga mjini kuna matuta 96 hatujui ni kwanini, lakini pia haya matuta mengine yanaharibu barabara, kuwe na upembuzi yakinifu kujua ni matuta gani yanastahili kuqepo barabarani" alisema diwani wa Maweni ambaye pia ni Naibu Meya wa jiji la Tanga.
Aidha walizitaka mamlaka hizo kushikisha wananchi kwenye maeneo ambayo wanapanga kufanya ujenzi ili kujua ni eneo gani sahihi ili kuepuka usumbufu unaotokea baadaye kwakuwa yapo maeneo ambayo barabara zimepita mashuleni jambo linasababisha ajali na vifo kwa wanafunzi.
"Kwa sasa tupunguze ujenzi wa mashule barabarani watoto wetu wanakufa kwa ajali, TANROADS wanatoa fesha nyingi sana kulipa fidia kwa watu waliojenga barabarani, ifike mahali tuwe tunapanda miti tu barabarani" alisema mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe.
Naye Meneja wa TARURA mkoani hapa alisema wataufanyia kazi ushauri wa wajumbe na kufafanua kwamba uwekaji wa matuta na rasta yamewekwa ili kuepusha ajali zinazotokea mara kwa mara ambazo nyingine husababisha vifo.
"Matatizo tunayoyapata hapa ni ajali, watu wanalalamika na tumefanya hivi kwa ajili ya kuzuia ajali hasa za bodaboda, tutayarekebisha matuta ili yawe rafiki katika maeneo yote ambayo yanalalamikiwa" alifafanua.
Aidha Katibt Tawala Mkoa wa Tanga Pili Mnyema alisema kuna uharibifu mkuwa wa barabara zinazotengenezwa unaofanywa na wananchi hivyo ni vema kutoa elimu kwa wananchi hao kuweza kuwa walinzi wa miundombinu naa atakayebainika achukuliwe hatua kali.
"Kwahiyo sisi tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba miundombinu ile inalindwa na kudumu kwa muda mrefu, baadhi ya barabara zimekuwa hazikai muda mrefu, na hii inachangiwa na baadhi ya wananchi kutokuwa na uelewa" alisema.
"Kwahiyo niwaombe wananchi, wanapoona kuna tatizo la uharibifu wa miundombinu watoe taarifa kwa mkuu wa Wilaya, kamati za usalama zipo ili waweze kuchukuliwa hatua na iwe fundisho kwa wengine, tukikaa kimya miundombinu itaendelea kuharibiwa na mwisho wa siku tutakuwa tukiilaumu serikali.
0 Comments