******************
Na Mwandishi Wetu
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), itatengeneza na kusimamia Sera ya Filamu itakayohakikisha kukua kwa utamaduni na kusaidia kuweka mazingira bora ya uwekezaji utakoimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na mataifa mengine.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo Usiku wa Juni 19, mwaka huu wakati wa Sherehe za Ufunguzi wa Tamasha la 25 la Filamu kwa Nchi za Jahazi (ZIFF) zinazoendelea kwa siku 9 katika viunga vya Ngome-Kongwe, Forodhani, Mjini Unguja.
Mhe.Othman amesema kuwa hiyo ni kutokana na uhalisia kwamba mwendelezo wa harakati za Tamasha la Filamu na Maonyesho ya shughuli mbali mbali za Utamaduni wa Asili wa Mzanzibari na Nchi za Jahazi, zinaitambulisha Zanzibar duniani na kwamba ni miongoni ma fursa muhimu za kuikuza Nchi kiuchumi.
Ambapo amesema matukio ya kitamaduni, kama vile Tamasha la ZIFF linaloendelea sasa nchini hapa, huwezesha ubadilishanaji wa moja kwa moja wa mawazo, mila, silka na maongezi kati ya jamii za watu tofauti, hasa kwa kuzingatia uzuri na upekee wa Visiwa vya Zanzibar tangu asili uliotokana na historia ndefu katika ulimwengu wa ustaarabu.
Mhe.Othman amebainisha kuwa Binaadamu daima hujisikia vyema anapoweza kutambulisha ustaarabu wake na wengine wakasifia na kuweza kujifunza kutoka kwake, ambapo hiyo ni katika siri za Tamasha la Utamauni wa Nchi za Jahazi.
"Katika kujifunza tunapata kubadilishana mawazo, ujuzi, ufahamu na elimu, vitu ambavyo ni muhimu kwa maendeleo ya binadamu na ni sehemu muhimu sana ya kuenzi na kutukuza utu wetu katika njia ya mshikamano na hivyo kuwa kielelezo cha haki, amani na ustawi wa kimataifa", amesisitiza Mheshimiwa Othman.
Aidha amesema kuwa filamu zinazungumza lugha moja; ni muhimu na zina maana sawa kwa ulimwengu na watu wote, bila kujali asili zao za kitaifa, kitamaduni au kijamii ambapo pia ni njia moja maarufu ya sanaa za kisasa, zinazovunjavunja vizuizi baina ya watu, mataifa na tamaduni, huku zikisisitiza maadili, hisia na utashi ambao mwanadamu daima anapenda kuudhihirisha kupitia kubadilishana mawazo.
Katika nasaha zake Mheshimiwa Othman ametoa wito kwa wageni ambao ni kutoka ndani na nje ya Afrika, wakiwemo washiriki kutoka Oman,Falme za Kiarabu, na Umoja wa Ulaya, kutenga muda na kutembelea vivutio vya Zanzibar kwa ujumla, na kujionea urithi na utajiri wa utamaduni wa visiwa hivi,huku akisisitiza kwa kusema, "haya ni maendeleo ya kipekee ya Tanzania ya leo na ndipo tunapoona umuhimu wa kuwa na Tamasha la Kimataifa".
"Kupitia mahusiano haya wakaambukizana utamaduni na urithi wa dunia; ndiyo maana ni furaha kubwa kuona kwamba kwa kupitia Tamasha hili tunaendeleza nguzo hiyo moja muhimu ya utu na urithi wa binadamu", ameongeza Mheshimiwa Othman.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Bi Tabia Maulid Mwita amesema kuwa daima amekuwa akifahamisha tija ya ziada iliyopo katika ufanikishaji wa Tamasha la Filamu la ZIFF hapa visiwani, ikiwemo upeo mpya wa ubunifu baina ya watengeneza- filamu wa Tanzania, na kwamba ikitokea shaka yoyote dhidi ya mila na silka za asili, ni vyema watu wasisite kuibuka na kushauri ili kunusuru utamaduni uliojaa ustaarabu wa Kizanzibari.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF, Bw. Hassan Mitawi amesema kuwa filamu ni chombo muhimu cha kuelezea maisha na utamaduni wa watu na jamii yeyote inayohitaji maendeleo katika nyanja zote za maisha zikiwemo za uchumi.
Akieleza mafanikio ya ZIFF kwa Kpindi cha Miaka 25 tangu kuasisiwa kwake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamasha hilo hapa Visiwani, Profesa Martin Mhando amesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni, tasnia ya filamu ya Tanzania na Afrika kwa ujumla imestawi, ambapo filamu bora zaidi za Kiafrika na hata za Kitanzania zinaonekana katika orodha ya Tuzo za Kimataifa.
Nae Mkurugenzi Mkuu a Tamasha hilo, Prof. Martin Mhando alibainisha kuwa, Watengeneza filamu wa Kitanzania kupitia Tamasha hilo, watapata fursa adhimu ya kutazama filamu kutoka nchi mbalimbali zilizochaguliwa vyema, zenye mandhari na mitindo mbalimbali, ili kujifunza zaidi.
Aidha, alisema kuwa, Mwaka huu takribani filamu 3450 kutoka Nchi 33 ziliingia katika mchujo na hatimaye 101 zilipata kupita na kuoneshwa kupitia Tamasha hilo.
Watu Mashuhuri na Viongozi mbali mbali wa Serikali na Asasi za Kiraia wamejumuika katika tukio hilo.
0 Comments