Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais leo Juni 7, 2022 jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Switbert Mkama.
Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais wakiimba wimbo wa Mshikamamo ‘Solidarity forever’ kabla ya kuanza kwa kikao na Katibu Mkuu Bi. Mary Maganga leo Juni 7, 2022 jijini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Elisha Msengi akitoa neno la utambulisho kabla ya kuanza kwa kikao na Katibu Mkuu Bi. Mary Maganga leo Juni 7, 2022 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi Ofisi ya Makamu wa Rais kabla ya kuanza kwa kikao leo Juni 7, 2022 jijini Dodoma.
*******************
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga amepongeza watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa utendaji kazi wao ambao umeleta mafanikio makubwa.
Ametoa pongezi hizo leo Juni 7, 2022 jijini Dodoma wakati alipofanya kikao na watumishi hao kwa lengo la kukumbushana wajibu wao katika utekelezaji mzuri wa majukumu yao katika kipindi cha mwaka uliopita.
Aliwapongeza kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha ambao umewezesha kuandaa na kukamilisha Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Kitabu cha Historia ya Muungano na Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira wa mwaka 2022-2032.
Aidha, pamoja na pongezi hizo Bi. Maganga alisema ni wajibu wa kila mtu mtumishi kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa elimu yake, uwezo wake na kwa taaluma yake na hivyo kuleta tija katika utendaji kazi.
“Ndugu zangu tufanye kazi kwa kujitoa na kwa weledi kila mtu ana nafasi yake na kuna wengine huwa wanatumbia kazi ni wito, kazi ni sadaka, kazi ni ibada kwa hiyo tujitoe,” alisisitiza.
Pia alisema mtumishi wa Serikali ana wajibu wa kutunza kumbukumbu za nyaraka mbalimbali zikiwemo Sera, Miongozo ili vizazi vijavyo vipate ufahamu wa nini kimefanyika.
Alitolea mfano wa nyaraka za shughuli za Muungano ambazo Ofisi ya Makamu wa Rais inaratibu na kusema hatua hiyo itasaidia kujenga uelewa kwa vizazi vijayo kuelimika.
0 Comments