Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Dennis Londo (Mb) akizungumza na Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma na wajumbe wa kamati yake wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi Singida.
Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Selemani Shindika akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kampasi hiyo mkoani Singida.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) wakimsikiliza Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Selemani Shindika akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kampasi hiyo mkoani Singida.
Mwonekano wa jengo la Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) Kampasi ya Singida.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) wakiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Deogratius Ndejembi na Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania mara baada ya na kamati hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida.
***********************************
Na. Veronica E. Mwafisi-Singida
Tarehe 06 Juni, 2022
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Dennis Londo (Mb) amesema kamati yake imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) Kampasi ya Singida na kuipongeza Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuitumia taasisi yake ya Watumishi Housing Investment (WHI) kujenga kampasi hiyo kwa kiwango bora.
Mhe. Londo amesema hayo mkoani Singida wakati wa ziara ya kikazi ya kamati yake ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa iliyolenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kampasi ya Chuo cha Utumishi wa Umma mkoani humo.
“Tunaipongeza Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa kuona umuhimu wa taasisi zake kushirikiana kiutendaji, ushirikiano ambao umetoa fursa kwa Watumishi Housing Investment kupewa kandarasi ya kujenga Chuo cha Utumishi wa Umma, Kampasi ya Singida, huu ni mfano mzuri wa kuigwa na taasisi nyingine,” Mhe. Londo amefafanua.
Ameongeza kuwa, kutokana na ufanisi wa kiutendaji wa WHI ni vema Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Serikali kwa ujumla kuona namna bora ya kuitumia taasisi hiyo katika ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja ujenzi wa nyumba kwa ajili ya makazi ya watumishi wa umma.
Mhe. Londo amesema, WHI imefanya kazi nzuri kwenye ujenzi wa Kampasi hiyo ya TPSC Singida kwani Kamati yake ilitembelea miradi mingine inayojengwa na taasisi nyingine za Serikali ambapo ilibaini kuwa fedha imeshalipwa lakini miradi hiyo haijakamilishwa.
“Nitoe rai kwa WHI kuendelea na kasi hii nzuri ya ujenzi wa miradi ya Serikali ili muwe mfano bora wa kuigwa na taasisi nyingine zinazojishughulisha na ujenzi wa majengo ya Serikali pamoja na makazi ya watumishi wa umma,” Mhe. Londo amesisitiza.
Awali, akieleza nafasi ya TPSC na WHI katika ujenzi wa mradi huo wa TPSC Kampasi ya Sindida, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Deogratius Ndejembi amesema mteja ni TPSC na mjenzi ni WHI ambapo taasisi zote hizo zipo chini ya ofisi yake.
Mhe. Ndejembi ameeleza kuwa, ofisi yake inapenda taasisi zilizo chini yake zishirikiane kiutendaji ili iwe rahisi kutekeleza jukumu la usimamizi wa miradi yote kwa ufanisi mkubwa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Emmanuel Shindika amesema chuo chake kimeamua kujenga Kampasi ya Singida ili kuokoa milioni 87 ambazo zimekuwa zikilipwa kila mwaka kwa ajili ya kukodi majengo ya kuendesha shughuli za kila siku za kampasi hiyo ya Singida.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) imepewa dhamana ya kusimamia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na taasisi zilizo chini yake.
0 Comments