Ticker

6/recent/ticker-posts

JENERALI MABEYO AWEKA JIWE LA MSINGI,UJENZI UWANJA WA GOFU,HOTELI YA NYOTA TANO NA KITUO CHA MICHEZO DODOMA.



*****************************

Zena Mohamed,Dodoma.

MKUU wa Majeshi ya ulinzi nchini,Jenerali Venance Mabeyo,ameweka jiwe la msingi wa ujenzi wa Mradi wa uwanja wa Gofu,hoteli ya nyota tano pamoja na kituo Cha michezo katika eneo la Ihumwa Jijini Dodoma ambao una thamani ya Shilingi bilioni 59.7ambapo amesema lengo la Mradi huo ni kuongeza Pato la Taifa.

Mabeyo ametoa kauli hiyo jijini hapa leo wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi hilo huku akizitaka Mamlaka mbalimbali wakiwemo Wadau wa maendeleo kuwekeza jijini hapa kwa manufaa ya Umma.

"Lengo la kujenga viwanja vya michezo ni pamoja na kuisapoti serikali katika kuendeleza michezo hapa nchini,ili watanzania wazidi kuipenda michezo pamoja na kupanua wigo wa kushiriki mashindano ya kimataifa,

"Hivyo niipongeze kamati ya Ujenzi wa uwanja huu iliochini ya Mwenyekiti Brigedia Hassan Mabena imefanya kazi nzuri ya ubunifu wa uwanja huo,”amesema.

Jenerali Mabeyo ameeleza kuwa uwanja huo ni wa kwanza kujenga jijini Dodoma lakini ni wa pili wa mchezo wa Gofu kujengwa na Jeshi hilo hapa nchini,ambapo wa kwanza ni ule wa Gofu uliopo Lugalo Mkoani Dar es Salaam.

“Huu ni mwanzo mzuri katika kuimarisha mchezo huo hapa nchini ambapo mchezo huo umeanza kuwa maarufu sana na tumeanza na uwanja huu lakini lengo letu ni kujenga viwanja kama hivi nchini nzima ili kusisimua hamasa ya mchezo huo,"amesema.

Ameeleza kuwa michezo ina umuhimu mkubwa kwa rika zote kiafya hivyo kukamilika kwa uwanja huo utasaidia watu kukusanyika katika eneo hilo na kupata burudani huku jeshi likiingiza kipato na kusaidia kuinua uchumi wa jeshi.

Pamoja na hayo amesema kutakua na ujenzi wa kituo cha michezo mingine katika eneo hilo ambalo litakuwa na viwanja vya michezo mbalimbali pamoja na ujenzi wa hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota tano.

Ambapo amesema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo utasaidia kuongeza uchumi katika jiji la Dodoma kwani itatoa ajira za moja kwa moja na za muda

Hata hivyo amewataka Majenerali na Maofisa wa Jeshi hilo kujifunza kucheza mchezo wa Gofu na michezo mingine ili wapatapo muda wa kushiriki mashindano ya nje wajitokeze kwa wingi kama wanavyofanya wanamichezo wengine.

“Kuna mashindano ya ngazi mbalimbali Jeshini,hivyo wakijifunza michezo itasaidia kutoa ushindano pindi mashindano yanapotokea,"alisema.

“Nimefurahishwa na kituo hiki kitakuwa pia na academy kwa mchezo wa Gofu hii naimani itasaidia sana kukuza mchezo huo hapa nchini na itakuwa nchi ya tatu kwa kuwa na academy” Amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi ya ulinzi mstaafu,Jenerali George Waitara amesema kuwepo kwa miradi hiyo ni fursa kwa Nchi ya Tanzania katika kukuza uchumi ambapo amesema Jenerali Mabeyo ameacha alama kwa Taifa kwa Mradi huo mkubwa.

Ambapo amesema yalikuwa ni matamanio yake ya muda mrefu ya kuwa na uwanja mkubwa wa gofu Dodoma na kila kanda ili kuinua ari ya mchezo huo nchini.

“Namshukuru Jenerali Venance Mabeyo alituahidi kuwa lazima ataanza uwanja wa Gofu na ametimiza ahadi yake na sasa uwanja huo unaanza kujengwa ambao utakuwa ni hazina kubwa katika kukuza mchezo huo h nchini,"Amesema Jenerali Waitara.

Aidha amewaasa watanzania kutoogopa mchezo huo kwani hauna gharama kubwa kama watu wanavyoongea na kubainisha kuwa katika kituo hicho cha michezo itakuwa kama chuo cha mchezo wa Gofu nchini.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi huo ambaye pia ni Mkuu wa Tawi la Utawala Jeshi la kujenga taifa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema eneo hilo lina ukubwa wa ekari 523 ambapo maandalizi yameanza ambapo mbali na ujenzi wa uwanja wa Gofu vitajengwa viwanja vya vingine mbalimbali ikiwamo Hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota tano.

Brigedia Jenerali Mabena,amesema kuwa ujenzi wa kituo hicho cha michezo utagharimu zaidi ya bilioni 59 na kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho utainua hadhi ya makao makuu ya nchini na kupitia kituo hicho kitawaongezea mapato kupitia fedha za viingilio na ada.

Aidha ametaja baadhi ya viwanja vitakavyojengwa katika kituo hicho ni Uwanja mkubwa wa Gofu, uwanja wa mpira wa Miguu wenye uwezo wa kuchukua watazamaji elfu kumi(10,000), uwanja wa Tenis, Mpira wa Kikapu, Bwawa kubwa la kuogelea lenye hadhi ya Olimpiki na kituo cha michezo ya watoto.

Post a Comment

0 Comments