Ticker

6/recent/ticker-posts

JAMII YA KIFUGAJI SASA RUKSA KUHAMIA MSOMERA KWENYE MAKAZI YA KUDUMU NA MAISHA BORA.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana akielekeza jambo wakati wa ukaguzi.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana akikagua mradi wa maji.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima alifafanua kuhusu miradi inayotekelezwa.


**************************

Na Hamida Kamchalla, HANDENI.


WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana ameeleza kuwa wakati wowote kuanzia sasa wananchi waishio katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wataanza kuhamia katika makazi mapya yaliyopo kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.

Dkt. Chana alitoa kauli hiyo alipofanya ziara ya kukagua hali ya utayari wa miundombinu ya makazi, maji, umeme, madarasa ya shule za msingi na sekondari, zahanati, majosho kwa ajili ya mifugo pamoja na barabara katika kijiji hicho.

Aidha alisema, ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu hiyo ambayo imekamilika na kwamba wananchi wote waio tayari kutoka Ngorongoro wanaweza kuhamia kwa hiari muda wowote kuanzia sasa.

“Tumekuja kukagua hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa makazi, na huduma za kijamii kwa wananchi watakaohamia hapa, nimeridhika sehemu kubwa ya miundombinu imekamilika, muda wowote kuanzia sasa Wanangorongoro waliojiandikisha kwa hiari watahamia hapa kuendelea na maisha ili kupisha shughuli za uhifadhi ndani ya eneo” alifafanua.

Alieleza kuwa pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa nyumba 100 na huduma zingine za kijamii, serikali bado inajipanga kuanza awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba nyingine za makazi 400 kwa ajili ya kuwezesha wananchi wanaoendelea kujiandikisha kwa hiari kuhamia Msomera, huku akiwataka wananchi wa maeneo hayo kuwapa ushirikiano.

"Wale ambao wapo tayari wanaanza kuingia, kwahiyo naomba tuwapokee tushirikiane nao, na hili zoezi ni endelevu, wapo wale ambao wapo tayari kuhamia kwa hiari, hapa tuna nyumba 100 lakini bado zinaongezeka nyingine 400,

"Maana yake, kuna tumu nyingine ambazo zinaendelea kuhamia hapa, kwahiyo sisi tunaendelea na maandalizi kuhakikisha kwamba eneo hili hatimaye linalindwa kwa ajili ya masuala ya uhifadhi kwasababu hivi sasa kumekuwa na mijadala kuhusiana na suala zima la wanyama" alifafanua.

Hata hivyo alisisitiza kwamba, "ni wakati muafaka sasa kwamba hili tatizo la wanyama, maeneo yale ambayo yana wanyama, wananchi wanapata eneo hususani hawa wanaotoka Ngorongoro kuja hapa ili wapate maisha bora na mazuri bila kuwa na kero ya wanyama waharibifu na wakali".

Awali akiwa wilayani Korogwe kwenye kikao cha Jumuiya ya Wanawake Ccm mkoani humo, Dkt. Chana alisema Wizara yake inatarajia kutoa namba maalumu kwa wananchi kwa ajili ya kudhibiti wanyama waharibifu kama tembo kuingia kwenye makazi ya watu.

"Kutokana na adha ya tembo kuingia kwenye makazi na kufanya uharibifu wa mazao, tumeamua kuja na mpango huo ili kuharakisha suala la kudhibiti wanyama hao wasiweze kuleta madhara, tunakwenda kumaliza tatizo la tembo kuvamia makazi yetu hususani yaliyopo jirani na hifadhi kwa kuwa na namba ambayo mwananchi akipiga anaweza kupata msaada kwa haraka" alisema.


Naye mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima alielza kuwa Mkoa huo umeshaandaa mazingira ya kuwapokea wananchi wa Ngorongoro, hali ya kiusalama iko shwari na tayari vyumba saba vya madarasa, maabara, Bweni na majosho kwa ajili ya mifugo yamekamilika sambamba na usambazaji wa huduma za maji, umeme na mawasiliano ya barabara.

Post a Comment

0 Comments