***********
Naibu waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Pauline Gekul (Mb) amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inajali kila kitu kinachomwezesha Mtanzania kuishi kwa amani huku akishiriki Michezo na Burudani kwa kadri ya uwezo wake.
Mhe. Gekul amesema hayo Juni 19, 2022 alipowaongoza wakazi wa jiji la Dar es Salaam katika maadhimisho ya nane (8) ya siku ya YOGA kimataifa yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru, ambapo amesema mazoezi ya YOGA yameonekana kuwa na manufaa sana yanapofanyika kwa utaratibu na utaalamu kiasi cha kutibu na kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
“Ndugu washiriki, nitumie nafasi hii kuwataka watanzania kuyachukulia mazoezi ya YOGA kwa umuhimu wake ili waweze kujenga umoja, mshikamano na kuboresha afya za mwili na akili pamoja na kusaidia kupunguza msongo wa mawazo" amesisistiza Mhe. Gekul.
Naye Balozi wa India nchini Tanzania Mhe. Binnaya Srikanta Pradhan ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwa bega kwa bega katika maadhimisho yote yaliyofanyika nchini Tanzania tangu Umoja wa Mataifa kupitia UNESCO kuitambua siku ya YOGA duniani, mnamo Desemba 11 , 2014.
0 Comments