Ticker

6/recent/ticker-posts

FEDHA ZA RAIS SAMIA KUBORESHA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA DODOMA - WAZIRI UMMY


*************************

Na. Catherine Sungura,WAF-Dodoma

Serikali ilitoa Shilingi Bilioni 263 ya fedha za ahueni ya UVIKO-19 ili kuboresha Hospitali za rufaa za mikoa kati ya fedha hizo hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma ilipewa kiasi cha bilioni 4.6 ambazo zimeweza kujenga jengo la wagonjwa mahututi (ICU) litakalokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 50 kwa wakati mmoja pamoja na ununuzi wa vifaa tiba.

Hayo yamebainiashwa leo na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati alipotembelea Hospitali hiyo kujionea utekelezaji wa fedha hizo ambapo kunajengwa jengo la wagonjwa mahututi(ICU), jengo la Radiolojia (CT-Scan), nyumba ya mtumishi pamoja na ukarabati wa jengo la huduma za dharura (EMD).

Amesema kutokana na jengo la wagonjwa mahututi (ICU) linaendelea vizuri na hivyo litasaidia kuongezeka kwa vitanda vya wagonjwa mahututi hadi kufikia wagonjwa 50 kutoka wagonjwa 18 hapo awali.

“Fedha hizi tulizowezeshwa na Rais Samia Suluhu Hassan, sasa Wizara ya afya kipaumbele chetu ni ubora wa huduma, hivyo kutokana na vitanda hivyo tutaweza kuwahudumia wagonjwa mahututi 50 ikiwa ni utekelezaji wa maono na dhamira ya Mheshimiwa Rais”. Amesema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema kwa jengo la Radiolojia ambalo litawekwa mashine ya CT-Scan ambapo huduma hiyo haikuweppo hapo awali na hivyo itaweza kupunguza mzigo kwa wakazi wa Dodoma ambao walikuwa wanaenda kupata vipimo hivyo kwenye hospitali ya Benjamini Mkapa.

“Hospitali hii kwa mwezi wanapata wagonjwa 75 hadi 100 ambao wanapaswa kufanyiwa kipimo cha TC-Scan, hivyo huduma hii itawawezesha wananchi kupata kwa bei rahisi na kuwaondolea usumbufu hadi hospitali ya kanda ya Benjamini Mkapa”. Aliongeza Waziri Ummy.

Kwa upande wa ukarabati wa jengo la huduma la dharura (EMD) Waziri huyo amesema huduma zote za dharura zitapatikana katika eneo moja hivyo Serikali imeweza kuboresha huduma za wagonjwa dharura kwani kutokuwa na huduma hizo unaweza kupoteza maisha ya watu.

Hata hivyo Waziri Ummy amekiri kutokutosha kwa vitanda kwenye huduma za dharura kutokana na ongezeko la watu pamoja na ufinyu wa eneo la hospitali hiyo kuahidi kufanya mazungumzo jiji la Dodoma ili kujenga hospitali nyingine ya rufaa ya Mkoa ili hospitali ya rufaa ya mkoa ibaki kutoa huduma za kibingwa na kuweza kupunguza mrundikano wa wagonjwa.

Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt.Ernest Ibenzi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa ya miundombinu na vifaa tiba katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambayo yameweza kuboresha huduma za afya.

Dkt. Ibenzi amesema majengo hayo yatasogeza huduma zaidi kwa wananchi na hivyo kuondoa mrundikano wa wagonjwa hospitalini hapo na kuahidi wataendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuimarisha huduma za afya.

Post a Comment

0 Comments