Ticker

6/recent/ticker-posts

CHUO KIKUU CHA MZUMBE KUFUNGUA TAWI TANGA

MKUU wa Mkoa wa Tanga Adam Malima akizungumza mara baada ya mazungumzo hayo.
MKUU wa Mkoa wa Tanga Adam Malima akiongoza kikao cha majadiliano ya kuanzishwa kwa Kampasi ya Chuo cha Mzumbe Mkoani hapa na uongozi wa chuo hicho

*******************

Serikali imetenga Sh bilioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Tanga.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Lughano Kusihika amesema hayo wakati yeye na ujumbe wake ulipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa ajili ya mazungumzo na kujadiliana eneo la kujenga chuo hicho.

Alisema serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeamua kwamba Chuo Kikuu cha Mzumbe kishiriki katika kuanzishwa kwa chuo kikuu katika Mkoa wa Tanga na kwamba fedha kwa ajili ya shughuli hiyo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia (IMF) kwa ajili ya kuboresha miundombinu na rasilimali watu na Mzumbe ni moja kati ya vyuo ambavyo vimepata fursa hiyo.

“Kwa ajili ya kuanzisha kampasi ya Tanga zimetolewa Sh bilioni 15 kwa hiyo tuko katika maandalizi ya kufanya shughuli hiyo na sisi kama Mzumbe tumefurahi kwa heshima ambayo tumepewa Mkoa wa Tanga ya kuja kuanzisha kampasi yetu hapa.

“Mkoa wa Tanga wote tunaufahamu ni mkoa mkubwa ambao una mambo mengi na huko nyuma ulikuwa ni maarufu sana kwa ajili ya viwanda na wote tunajua kwamba serikali yetu inataka kujenga uchumi wa viwanda, kwa hiyo sisi ambao tuko katika vyuo vikuu tunatakiwa tushiriki kikamilifu katika shughuli hii na mradi wenyewe kwa ujumla wake unafadhiliwa na IMF kwa mageuzi ya kiuchumi,” alisema.

Alitaja lengo kubwa la serikali ni kuangalia namna gani vyuo vikuu vitashirikiana na jamii katika maeneo mbalimbali kuendesha programu na kujenga uwezo kwenye maeneo hayo na kufanya shughuli ambazo zitaleta mageuzi.

Profesa Kusihika alisema bado wanaendelea na majadiliano ya kupata eneo ambalo wanaweza kuanza ujenzi ambapo alifafanua zaidi lengo la serikali ni kuanzisha kampasi na kuikuza halafu huenda huko mbeleni ikafika mahala ikawa ni chuo kikuu kinachojitegemea.

“Kwa hiyo tunawaomba sana wakazi wa Mkoa wa Tanga na viongozi wao, wapokee hili wazo zuri kutoka serikalini kwa sababu lina maslahi makubwa na mapana kwa nchi yetu maana sasa hivi serikali inafanya mapinduzi makubwa katika mkoa huu ambapo inakwenda kuwekeza kwenye bandari pia tunajua bomba la mafuta linalotoka Hoima litakuja kuingia Tanga.

“Hayo yote yanaonyesha kwamba tutakuwa na shughuli nyingi za kiuchumi lakini tunahitaji kuwatayarisha watu wetu ili waweze kushiriki katika kutumia fursa hizo na maendeleo ya mkoa wa Tanga na Tanga ikiendelea inachangia kwenye maendeleo yetu,” alisema Profesa Kusihika.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima alisema wamefanya mazungumzo na uongozi wa kujua wanafanya lakini fedha zimeshatoka kwa ajili ya kuanzisha chuo kikuu hicho mkoani hapa.

“Tulichokunaliana ni kwamba mwezi ujao Julai hadi Agosti, tutaanzisha Chuo Kikuu cha Mzumbe hapa Tanga kwenye maeneo ya makazi ya muda wakati tunafanya ujenzi wa makazi ya kudumu kwa sababu kuna maeneo matatu Mkinga, Muheza na Tanga.

“Tulikuwa tunajadiliana maeneo kwa sababu mwanzo ilikuwa fikra kwamba lipatikane eneo la ekari kama 200 lakini ukipata ekari 200 leo baada ya miaka 20 utahitaji eneo la ekari 300-400 huna sehemu ya kupanua Tukasema hapana ndiyo maana nimewaita wakuu wangu wa wilaya wa maeneo hayo, Mstahiki Meya, Katibu Tawala na Ofisa Elimu wa Mkoa kwa sababu ni jambo ambalo kimkakati kwa masaa haya yanayokuja tunataka tupate eneo ambalo wote hapa tutaliangalia kwa pamoja,” alisema Malima.

Pamoja na mambo mengine, Malima alisema walikuwa na mkutano na Katibu Mkuu wa Mifugo wakakubaliana kutakuwa na Kitivo cha Mifugo ili kuendana na mahitaji ya mifugo, Kitivo cha Mambo ya Uchumi wa Buluu na mambo mengi ambayo bado wanawaza ili chuo kiwe kinafundisha masomo mahsusi ambayo yanaendana na mahitaji ya kanda hiyo na maeneo mengine ya Tanzania kwa ujumla.

“Tumekuwa na mkutano mzuri ambao tunaamini kwa maamuzi haya Tanga sasa itapata chuo kikuu na fikra ni kwamba baada ya miaka 10 kiwe ni chuo kikuu kinachojitegemea.

“Tunawashukuru uongozi kwa kutufikiria sisi Tanga kwanza kama ni sehemu ya kuja kuweka tawi lao nataka niwahakikishie Wanatanga kuwa huenda mwaka huu au mwakani tutakuwa kwenye makazi ya muda miaka miwili tutakuwa kwenye eneo mahsusi,” alisema.

Post a Comment

0 Comments