Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Makampuni na majina ya Biashara (BRELA), Bw.Meinrad Rweyemamu akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 13, 2022 mara baada ya kuzindua WIKI YA SURUHISHA NA BRELA yenye lengo la kutatua migogoro ya makampuni nchini.
**********************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imezindua WIKI YA SURUHISHA NA BRELA ambayo itakuwa maalumu kwaajili ya kukutana na wamiliki wa makampuni kwaajili ya kueleza kero na migogoro iliyopo kwenye kampuni na kuweza kutatuliwa.
Akizungumza wakati wakifungua zoezi hilo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Makampuni na majina ya Biashara (BRELA), Bw.Meinrad Rweyemamu amesema kumekuwa na wamiliki wa makampuni kutaifishwa pamoja na kuwepo kwa migogoro kwenye makampuni yao, hibyo kupitia WIKI YA SURUHISHA NA BRELA wataweza kupata suruhisho la migogoro inayowakumba.
"Kwenye Kampuni mwenye hisa hutokea amefariki huku ndugu hawafahamu kinachoendelea kwenye kampuni, hawafahamu zile hisa za marehemu ni mali kama mali zingine ambazo zinagawiwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine. Njoo katika wiki hii tutakuwa pamoja, tutaangalia haki yako ni ipi". Amesema Bw.Rweyemamu
Aidha amesema watakaa na wamiliki pamoja na wahusika kujadiliana na kupeana elimu mwisho wa siku kila mtu apate haki yake na kuondokana na migogoro ambayo imekuwa ikitokea kwenye makampuni mbalimbali.
WIKI YA SURUHISHA NA BRELA imeanza leo Juni 13, 2022 na kufikia tamati siku ya jumapili Juni 19,2022 hivyo basi wenye makampuni wametakiwa kufika eneo husika ambalo ni Makumbusho ya Taifa Posta Jijini Dar es Salaam ili waweze kutatuliwa changamoto zao.
0 Comments