Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu (kushoto) akimkabidhi mkoba wa vitendea kazi kwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) Prof. Ephata Kaaya (kulia)
Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu (kushoto) akipokea taarifa ya utekelezaji kutoka kwa Bodi ya Wadhamini iliyomaliza muda wake kutoka kwa Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Prof. Hamis Dihenga (kulia)
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Prof. Ephata Kaaya akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Picha ya pamoja Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
**********************
Na WAF – DAR ES SALAAM
Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu ameitaka Bodi mpya ya wadhamini katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kusimamia ubora wa huduma zinazotolewa katika Taasisi hiyo pamoja na kuweka mfumo mzuri wa kushughulikia malalamiko ya wananchi.
Waziri Ummy Mwalimu amesema hayo leo kwenye hafla fupi ya kuzindua Bodi mpya ya Wadhamini ya Taasisi hiyo Jijini Dar Es Salaam.
“Bodi mpya ya Wadhamini nataka mtambue kwamba mnayo kazi kubwa mbele yenu ya kuhakikisha Taasisi inatoa huduma zenye kiwango chenye Ithibati za Kimatafa tukiwa na lengo la kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma bora za kibingwa na kibobezi za Saratani hapa nchini” amesema
Waziri Ummy Mwalimu. Katika kuhakikisha Taasisi inaendelea kutoa huduma bora za matibabu Waziri Ummy ameutaka Uongozi wa Bodi kusimamia miradi iliyopo pamoja na kubuni miradi mipya ambayo itasaidia katika kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma za tiba ya Saratani nchini.
“Napongeza jitihada mbalimbali zinazofanyika katika kujenga uwezo wa huduma za kibobezi, uboreshaji wa miundombinu na vifaa tiba ili kuboresha huduma na hii ndio kazi ambayo Bodi mnatakiwa kuzifanya” Amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy ameitaja miradi ambayo Bodi hiyo inatakiwa kuisimamia ili iweze kukamilika na kutoa huduma bora ikiwemo, Miradi ya ujenzi pamoja na usimikaji wa mashine mpya ya kisasa ya uchunguzi wa saratani (PET CT Scan) pamoja na kiwanda cha Cycloton vyote kwa pamoja vikigharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 18.2 ambapo ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi huu Juni 2022 na usimikaji wa mashine kuanza mwezi ujao.
Ametaja miradi mingine kuwa ni ukarabati na usimikaji wa mashine mpya za MRI, Digital X-Ray, ukarabati wa jengo na ununuzi wa vifaa vya wodi ya wagonjwa mahututi (ICU), kukarabati na kusimika vifaa kwa ajili ya huduma za tiba mtandao (Telemedicine) zitakazogharibu Shilingi Bilioni 5.4 kutoka kwenye fedha za UVIKO-19.
Waziri Ummy ameitaka Bodi hiyo kuweka mipango madhibuti ya kutatua kero za wananchi pamoja kutatua changamoto zilizoikumba Taasisi katika kipindi cha nyuma ili ziwe chachu ya mafanikio ya utoaji wa huduma bora za matibabu.
Aidha Waziri Ummy Mwalimu ameipongeza Bodi iliyomaliza muda wake kupitia kwa Mwenyekiti wake Prof. Hamis DIhenga kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kuboresha huduma za saratani, ununuzi wa vifaa tiba pamoja na ujenzi wa miundombinu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi iliyomaliza muda wake Prof. Hamis Dihenga amesema katika kipindi cha uongozi wa Bodi yake waliweza kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi wa Serikali hivyo kuiwezesha Bodi kufanya kazi ambayo imeweza kuleta tija katika kuboresha huduma za tiba ya Saratani nchini.
“Katika kipindi cha uongozi wa bodi yangu tuliweza kuongeza huduma za tiba ya saratani kutoka aina mbili hadi kufikia kutoa tiba za aina sita za saratani” amesema Prof. Dihenga.
Naye, Prof. Ephata Kaaya Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Wadhamini ameahidi kuendeleza mazuri yote yaliyofanywa na Bodi iliyomaliza muda wake.
Prof. Kaaya amesema kupitia wajumbe wa Bodi yake watahakikisha wanasimamia vyema Taasisi hiyo na kushirikiana na Taasisi pamoja na wadau wengine kuhakikisha wanaboresha huduma ili wananchi waweze kupata huduma zote hapa hapa nchini pamoja na kuleta maendeleo ndani ya Taasisi hiyo.
0 Comments