******
Chuo Kikuu Ardhi (ARU), kupitia Taasisi yake ya Utafiti ya Nyumba wamebuni teknolojia ya ujenzi wa gharama nafuu kwa kutumia matofali yanayojengwa kwa kutumia udongo wa mfinyanzi, saruji na maji kidogo, ni matofali ambayo rafiki kwa mazingira.
Hayo yamebainishwa wakati wa maonyesho ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yanayoendelea kwenye viwanja vya kituo cha mikutano cha Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.
Akizungumza kuhusu teknolojia hiyo, Mhadhiri wa ARU Dkt. Given Mhina amesema matumzi ya tofali za aina hiyo zitasaidia kupunguza hewa ya ukaa duniani, kutunza na kuhifadhi mazingira.
“Tumekuja na teknojia hii kama sehemu ya jitihada ya kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa unaotokana na shughuli za ujenzi na mali ghafi zake kama vile saruji, mchanga na maji…. tunatumia udongo wa mfinyanzi na wakati mwingine vumbi linalotokana na utengenezaji wa kokoto,”
Alisema ujenzi wa nyumba kwa kutumia tofali hizo hauhitaji saruji, mchanga wala maji kwani zinafungamana zenyewe isipokuwa wakati wa kuweka nguzo za nyumba pekee.
Dkt. Mhina amesema hata wakati wa umaliziaji wa nyumba mtu aliyetumia tofali hizo halazimiki plasta ya saruji na mchanga badala yake mafundi watatumia mchanga na saruji kidogo sana kuziba mashimo na kisha mwonekano wa nyumba kuwa wa kuvutia.
Aidha faida nyingine ya matumizi ya matofali ya aina hiyo ni kutosababisha joto ndani ya nyumba kulinganisha na matofali mengine yaliyozoeleka kwenye shughuli za ujenzi.
“Tofali zinazotengenezwa kwa kutumia saruji na mchanga zinatabia ya kufyonza joto wakati wa mchana na joto hilo kutoka wakati wa usiku lakini mfinyanzi unaotumika kutengeneza tofali hizi unasababisha ubaridi kwasababu hauna tabia ya kufyonza joto,” alisema
“Ndiyo sababu kwenye chungu kilichotengenezwa kwa mfinyanzi ukiweka maji hata mchana wakati wa joto kali baada ya muda maji yanapata ubaridi na watu wengi wamekuwa wakitumia vyungu vya mfinyanzi kupata maji baridi,” alisema
Taasisi ya Utafiti wa Nyumba ya ARU imekuwa ikifanya tafiti kwa vifaa vya ujenzi vinavyopatikana hapa nchini na kwingineko duniani.
0 Comments