Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI UMMY - MSD MNUNUE DAWA KUTOKA KWA WAZALISHAJI WA NDANI NA NJE YA NCHI


*********************

Wizara kufanyia kazi maelekezo ya Mhe.Rais na Waziri Mkuu

Na. WAF - Dar es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameielekeza Bohari ya Dawa (MSD) kununua dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji wa ndani na nje ya nchi.

Maelekezo hayo ameyatoa leo Mei 5, 2022 mara baada ya kutembelea bohari hiyo jijini Dar es Salaam.

Aidha,Waziri Ummy ameitaka MSD kuripoti hali ya upatikanaji wa dawa aina 290 kwaajili ya matumizi angalau miezi minne na sio mwezi mmoja kama ilivyokuwa awali.

"Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetimiza wajibu wake kwakuwa inatoa kati ya Bil. 10 hadi 15 kila mwezi kwa ajili ya kununua dawa sasa na ninyi MSD mkatimize wajibu wenu." Amesema Waziri Ummy

Vile Vile Waziri Ummy amesema Wizara yake imeanza kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais wakati akipokea taarifa ya CAG kwa kuifumua MSD pamoja na maagizo ya Waziri Mkuu Hata hivyo ameitaka MSD ifanye maboresho makubwa katika eneo la huduma kwa wateja na shughuli za kanda kwa kufanya maboresho ya watumishi ili kuwezesha hospitali kubwa kununua dawa MSD badala ya kununua dawa kutoka kwa watu wa kati.

Waziri Ummy amesema MSD inatakiwa kufuata Sheria kwa kuzingatia mambo matatu ambayo ni thamani ya fedha, ubora wa bidhaa (Dawa) pamoja na muda wa kufikisha bidhaa kwa wahitaji.

"Watanzania wanahitaji kuona bidhaa za Afya kutoka MSD zenye ubora, salama na za gharama nafuu zinapatikana za kutosha." Amesema Waziri Ummy

Vile vile Waziri Ummy amesema MSD iendelea kujenga viwanda vya Dawa na vile vilivyoanzishwa vinakamilika hatua hii itasaidia kupunguza muda wa kuagiza dawa hadi ifike nchini lakini pia kubadilisha shillingi kuwa Dola pamoja na kuzingatia ubora.

"Mwisho nawataka watumishi wa MSD kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu za nchi katika utekelezaji wa majumu yenu ikiwemo taratibu za manunuzi ya umma." Amesema Waziri Ummy

Kazi ya MSD ni kununua, kutunza, kusambaza na kuzalisha bidhaa za Afya kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Serikali.

Post a Comment

0 Comments