Naibu Waziri Katambi akisalimiana na Mkuu wa chuo hicho Joyria Msuya Mara baada ya kuwasili chuoni hapo.
Naibu Waziri Katambi baada ya kuzindua chuo hicho kwa niaba ya Waziri Joyce Ndalichako.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana, na Watu wenye Ulemavu, Patrobas Katambi akiwa kwenye kwenye karakana ya mashine za cherehani na vijana wenye ulemavu katika chuo cha ufundi na marekebisho kwa watu wenye ulemavu, Kanda ya Kaskazini, kilichopo mtaa wa Masiwani jijini Tanga.
***************
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
VIJANA wenye ulemavu 474 mkoani Tanga watanufaika kwa kupatiwa elimu ya ujuzi bure ili kuwawezesha kujikwamua kimaisha na kuondokana na hali ya utegemezi.
Hayo yalibainishwa juzi na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Patrobas Katambi wakati akizindua Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu (Kanda ya Kaskazini kilichopo mtaa wa Masiwani jijini Tanga.
Naibu Waziri huyo alisema Wizara mbili zitashirikiana kuhakikisha vijana hao wanalipiwa ada na serikali, hivyo ni muhimu kwa wazazi na walezi wenye vijana walemavu kuwapeleka kuwaandikisha katika chuo hicho kwani zipo fedha za mfuko wa maendeleo ya vijana ambazo zinawalenga wao.
"Wapo vijana ambao Ofisi ya Waziri Mkuu inawasomesha, nitahakikisha tunashirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia tutoe fursa ya mafunzo stadi kwa vijana na wenye ulemavu 474 hapa, ambao watalipiwa ada na Ofisi ya Waziri Mkuu na katika kufanikisha hili vifaa ambavyo vitatolewa kwa awamu nyingine, tutahakikisha piia vinaletwa na hapa" alisema.
Aidha alibainisha kwamba serikali imedhamiria kufufua na kufungua vyuo hivyo ambavyo katika Mikoa sita nchini huku akitoa wito kwa wananchi kutumia fursa ya kufunguliwa kwa kuwapeleka vijana wao wenye ulemavu lakini pia wasio na ulemavu kwakuwa vinatoa mafunzo kwa mfumo wa elimu shirikishi.
"Rais amedhamiria kufungua vyuo hivi, tuwapeleke wanafunzi wakasome, siyo wale walemavu tu bali hata wazima ili wakasome, kwasababu hawa wa darasa la saba na kidato cha nne tunaowalenga hawakufichwa na wazazi/walezi wao wanapaswa kuandikishwa kwenye hivi vyuo wapate maarifa" alisema Katambi.
Naye mkuu wa chuo hicho Joyria Msuya alisema serikali ilianzisha vyuo hivyo ili kuwapa vijana wenye ulemavu elimu ya ufundi na uzalishaji mali kiushirika katika muelekeo wa kibiashara na baada ya mafunzo waweze kujitegemea katika jamii kwa kuajiriwa au kujiajiri hata kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali kiushirika.
"Kutokana na mafunzo hayo, mapato yaliyopatikana baada ya mauzo ya bidhaa walizozalisha yaligawanywa kwao ili waweze kujinunulia mahitaji yao na pia ununuzi wa zana za kufanyia kazi, kwa bahati mbaya mfumo huu ulipaya changamoto na hivyo matokeo hayakuwa mazuri kama ilivyotarajiwa" alisema Msuya.
"Vilevile wanafunzi wengi walikuwa wakishapata mafunzo katika vyuo vya awali hawakurudi tena kwenye karakana yetu ya Masiwani, hivyo kukosa elimu ya uzalishaji mali na ushirika, kulikuwa na idadi ndogo ya vijana wenye ulemavu waliojiunga kituoni kutoka kanda hii ya kaskazini na kufanya mpango mzima usimame" alibainisha.
Aidha alifafanua kwamba vyuo hivyo vilianzishwa mwaka rasmi machi 7, 1988, zikiwa na mafunzo ya fani tatu za useremala, ushonaji na ushonaji viatu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la NSSF Mashaji Mshombe alisema jukumu la msingi la kutoa na kusaidia jamii katika masuala muhimu kwa maendeleo ya Taifa, ikiwemo elimu na afya, hivyo kwa kutambua hilo moja ya vipaumbele vyao muhimu katika masuala ya kijamii ni usaidizi na kuzingatia msimamo wa serikali ya awamu ya sita.
"Tunaenedelea kuweka msisitizo wa kuongeza nguvu katika vyuo vya ufundi kadiri ambavyo Rais anavyosiditiza na ndiyo maana hatukusita pale ambapo kuna nafasi ya kusaidia hiki chuo cha Masiwani, tukaweka nguvu na ndiyo maana leo tuko hapa" alisema Mshombe.
Vyuo vya ufundi na marekebisho kwa watu wenye ulemavu nchini vinaendelea kutufuliwa upya na kuzinduliwa katika Mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Tabora, Mtwara, Singida na Tanga.
0 Comments