Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAWATAKA WAFUGAJI KUACHA KUFUGA KWA MAZOEA NA WAFUGE KWA TIJA


Katibu Mkuu Mifugo, Bw. Tixon Nzunda ( katikati ) akizungumza kwenye Kongamano la Maendeleo ya Tasnia ya Maziwa ( NDDC) lililo fanyika leo Mkoani Katavi lenye lengo la kuongeza tija kwenye sekta ya maziwa nchini. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Tamisemi Bw. Leo Mavika, wa pili kulia ni Bi. Leila Robin akimuwakilisha Msajili wa Bodi ya Maziwa, wa kwanza kushoto ni Bi. Skeeter Godwin kutoka Shirika la Dalberg na wapili kushoto ni Bw. Kayumba Torokoko mwakilishi Katibu Tawala Mkoa wa Katavi.


Afisa Uhusiano Benki ya CRDB Mpanda akielezea Fursa za Mikopo zinazotolewa na Benki kwa Wafugaji wakati wa Kongamano la Wadau wa Tansia Maziwa.


Meneja wa Ushirika wa Kilimanjaro Dairy Co-operative Joint Enterprise LTD Bw. Ernest Chad Haule akielezea baadhi ya Changamoto za Ushirika wakati wa Kongamano.


Baadhi ya wadau walioshiriki Kongamano la Wadau wa Tansia ya Maziwa lililofanyika leo katika ukumbi wa Mpanda mkoa wa Katavi.

...................................................

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Bw. Tixon Nzunda amewataka wafugaji kubadili mfumo wa ufugaji wa kuswaga mifugo na kutafuta maeneo ya kufugia kwa maana ya kuyanunua na kuyamiliki kutokana na idadi ya Mifugo waliyonayo.

Hayo ameyasema leo tarehe 31 mei 2022 wakati wa Kongamano la Wadau wa Tasnia ya Maziwa lililofanyika katika ukumbi wa Mpanda Hall wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Maziwa mkoani Katavi.

Katibu Mkuu Mifugo amesema uzalishaji wa maziwa ya ng'ombe umekuwa ni mdogo kutokana na umbali mrefu ambao ng'ombe amekuwa akitembea kutafuta Maji na Malisho.

"Ng'ombe wa Maziwa anatembea km 55 kwa siku,halafu unategemea atatoa maziwa mengi??haiwezekani, hatuwezi kuendelea na utaratibu wa kuswaga mifugo"

Bw. Nzunda amesema kuwa viwanda vya maziwa vimekuwa vikisindika maziwa chini ya uwezo uliokusudiwa kutokana na upatikanaji mdogo wa maziwa unaotokana na ufugaji wa kuswaga mifugo badala ya kufuga kisasa.

Nzunda amesema uwezo wa uzalishaji Maziwa ni chini ya Lita 23, Jambo ambalo ni aibu kwa Taifa ambalo ni la pili Africa kuwa na Mifugo Mingi.

" Ni aibu kwa Taifa Mifugo kubadilika kuwa sehemu ya migogoro badala ya neema na kuimalisha uchumi wa nchi"

Amesema kuwa Tanzania imekuwa ikitegemea maziwa kutoka Kenya na Uganda kutokana na uzalishaji mdogo wa Maziwa hapa nchini. Hivyo, amesema kuwa hatuna budi kufanya mabadiliko na kuweka mfumo rafiki wa kuwabadilisha wafugaji ili waanze kufuga kisasa na kwa tija.

Aidha, amesema kuwa, kupitia Kongamano la Wadau, wataalamu wataweza kuja na mbadala wa kuwasaidia wafugaji na kuweka mikakati endelevu ya upatikanaji wa malisho, maji pamoja na ufugaji wa kisasa.

Aidha, Bw. Nzunda aliwapongeza wafugaji kwa kuchangia asilimia 7.1 katika Pato la Taifa ingawa Sekta ya Mifugo ilikuwa na nafasi ya kuchangia asilimia zaidi ya 20.

Nzunda ametoa wito kwa Taasisi za Kifedha kuona changamoto hizi ni fursa ya kutafuta njia bora za kuweza kuwekeza katika sekta hii ya mifugo.

Awali Katibu Mkuu Mifugo alisema Mpango Mkakati wa kuboresha Sekta ya Mifugo unalenga katika uboreshaji wa huduma za ugani, kuimarisha Tafiti kwa kufanya tafiti za vitendo zaidi na kuboresha mbari za Mifugo.

Maeneo mengine ambayo mpango mkakati huo utazingatia ni pamoja na mifumo imara ya kuwawezesha wataalamu kuwajibika kwa wafugaji (Performance Contract) ili kutengeneza uwajibikaji kwa watumishi wa Umma na kupeleka huduma ikiyokusudiwa kwa Wafugaji.

Kwa upande wake, Bi . Leila Robin akimwakilisha Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania alimshukuru Katibu Mkuu kwa kushiriki katika Kongamano Hilo na kusema kuwa Bodi ya Maziwa ipo tayari kushirikiana na wadau mbimbali ili kutatua changamoto za wafugaji ikiwemo kutoa elimu ya ufugaji bora wa ng'ombe.

Unajua ukifuga kisasa na kwa tija kutapelekea kuzalisha maziwa mengi zaidi ili viwanda vvetu viweze kupata malighafi ya kutosha ya kusindika kulingana na uwezo uliokusudiwa wa Kiwanda.

Bw. Mahela ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) kutoa elimu ya ufugaji bora na wenye tija kwa wafugaji na kuwaunganisha na taasisi za kifedha ili kuwawezesha wafugaji kupata mikopo ili waweze kufuga ngo'mbe wa kisasa na kuachana na ufugaji wa asili.

Mahela ameiomba pia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) iwaelimishe na kupeleka msukumo kwa wasindikaji na wachakataji wengine wa Maziwa kupitia TBS ili kuweza kusindika maziwa kwa kufuata ubora na kuzingatia viwango vilivyothibitishwa.

Post a Comment

0 Comments