Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge akizungumza na wananchi wa Iguguno wilayani Mkalama wakati alipoongoza uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya polio uliofanyika leo Mei 18,2022
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge akiwa amempakata mtoto kabla ya mtoto huyo kupata chanjo hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge akiwa amempakata mtoto wakati mtoto huyo akipatiwa chanjo hiyo.
Wananchi wa Iguguno wakiwa kwenye hafla hiyo ya uzinduzi wa kampeni hiyo.
Kampeni hiyo ikizinduliwa.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Ibrahim Pazia akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ambapo aliwahimiza wananchi wa wilaya hiyo kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick akiwa amembeba mtoto wakati akisubiri kupata chanjo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Asia Messos akiwa amempakata mtoto wakati akipatiwa chanjo hiyo.
Viongozi mbalimbali wakiwa wamewapakata watoto wakati wakisubiri kupatiwa chanjo hiyo. Kutoka kushoto ni Katibu Tawala Wilaya ya Mkalama, Elizabeth Rwegasira, Diwani Viti Maalumu Kata ya Iguguno Mariam Hussein, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Sophia Kizigo na Dk.Ritha Willilo kutoaka Shirika la Afya Duniani (WHO)
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Cuthbert Kong'ola akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo.
Mwakilishi wa Wadau wa Sekta ya Afya Mkoa wa Singida Said Beleka akizungumza katika uzinduzi huo.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Honest Nyaki akichangia jambo wakati wa uzinduzi huo.
************************
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge ameongoza uzinduzi wa kampeni ya siku nne ya chanjo ya matone ya polio kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Kampeni hiyo ya siku nne ambayo imezinduliwa kimkoa Kata ya Iguguno wilayani Mkalama imeanza leo Mei 18 ambapo itamalizika Mei 21 mwaka huu.
Akizungumza wakati akizindua kampeni hiyo Mahenge alianza kwa kuelezea kazi kubwa iliyofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga bajeti kubwa kwa upande wa sekta ya afya ambapo kwa Mkoa wa Singida pekee kwa mwaka huu walipokea zaidi ya Sh.30 Bilioni huku hospitali za wilaya zikijengwa Ikungi, Manyoni, Mkalama na Singida DC kwa wakati mmoja na ndani ya mwaka mmoja.
Mahenge aliongeza kuwa katika mkoa huo katika sekta ya afya vinajengwa vituo vya afya 15 katika wilaya zote huku Iramba ikiwa na vituo vitano na kueleza kuwa hiyo sio kazi ndogo bali ni kazi kubwa anayoifanya Rais Samia Suluhu Hassan.
"Nimetangulia kuyasema haya ili kuonesha jinsi Rais wetu Samia Suluhu Hassan anavyo tujali watanzania na ndio maana leo tupo hapa tunazindua kampeni hii ya polio baada ya Serikali kutuwezesha" alisema Dk.Mahenge.
Alisema kazi kubwa ya serikali si kuangalia mienendo ya nchi pekee bali na ya nchi za jirani na ndio maana baada ya kugundua nchi ya Malawi kuna kirusi cha polia ndipo juhudi zilipoanza kuchukuliwa kwa kutoa kinga ya polia katika baadhi ya mikoa inayopakana na nchi hiyo lakini ili tuwe na uhakika serikali imeagiza chanjo hiyo ifanyike mikoa yote.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick alisema kwa mkoa huo wanatarajia kuwafikia watoto waliochini ya miaka mitano 286,736 na kuwa maandalizi yote yamekamilika.
Dk.Ludovick alisema chanjo hiyo itatolewa kwa siku tatu na lengo ni kufika kwenye maeneo yote na kuwa itafanyika nyumba kwa nyumba .
"Madhara ya ugonjwa wa Polio ni ulemavu wa ghafla wa viungo na usiotibika kwa hiyo ni muhimu sana kwa kila mzazi na mlezi wawatoe watoto wao wenye umri tajwa wapate chanjo hii ambayo ni salama" alisema.
Dk. Ritha Willilo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) aliwaomba wazazi kutoa ushirikiano wa kuwatoa watoto wao ili kupata chanjo hiyo na kusema kauli mbiu isemayo tone moja la chanjo ya polio linatosha kabisa kuwakinga watoto wetu dhidi ya ugonjwa wa kupooza wa polio.
Diwani wa Viti Maalumu (CCM) Kata ya Iguguno Mariam Hussein akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo alishukuru Serikali kusogeza huduma hiyo ya chanjo hadi walipo wananchi hivyo itaweza itaweza kuwafikia watoto wengi.
Kampeni hii inafanyika nchi nzima baada ya Serikali ya Malawi kutoa tamko mapema mwaka huu la kuwepo mlipuko wa Polio katika nchi hiyo baada mtoto mmoja kudhibitika kuwa na Polio na hivyo kuwa ni mara ya kwanza kwa bara ya Afrika kutokea changamoto hiyo baada ya kupita miaka mitano pasipo kuwepo na ugonjwa huo.
0 Comments