Na Zena Chitwanga,Dodoma.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Wamachinga nchini kuwa katika mwaka wa fedha unaoanza mwezi Julai Ofisi yake kupitia Tawala za mikoa na Serikali za mitaa itatoa Sh. Milioni 10 kwa kila mkoa kuwezesha shughuli za machinga nchini.
Rais Samia amesema hayo leo kwa njia ya simu wakati mkutano wa mafunzo ya Viongozi wa Machinga Tanzania (SHIUMA) ukiendelea Jijini Dodoma ambapo amewahakikishia kuwapa ushirikiano Wamachinga nchini kwa kufanya kazi zao bila shida kwenye mazingira mazuri.
"Nakushukuru Waziri kwa kuwapa Wamachinga Ofisi ambayo ni jengo la Serikali,nimesikiliza hotuba yao na nimefurahishwa,nawahakikishia ushirikiano na mazingira mazuri na ifikapo mwaka wa fedha unaoanza mwezi Julai nitatoa milioni kumi kwa Kila mkoa kuwezesha shughuli zao,"amesema
Awali akizungumza katika mkutano huo,Naibu Katibu Mkuu (SHIUMA) Joseph Mwanakijiji ameeleza kuwa kwa sasa wana mahusiano mazuri na serikali jambo ambalo linalosaidia Machinga anakuwa na mazingira mazuri na kuhakikisha anapangwa vizuri na kufanya biashara kwa uhuru.
Hata hivyo amesema wanachangamoto nyingi lakini kero ya miundombinu kwa baadhi ya masoko haiko sawa na kusababisha kiuchumi hawafikii malengo kwasababu baadhi ya miundombinu haiko sawa na kuhatarisha afya,ukosefu pia wa ofisi za Machinga na changamoto za kibajeti.
"Changamoto nyingine pamoja na stadi za biashara ,makazo bora,umilikishwaji wa maeneo ya machinga hivyo tunaomba kupewa barua ya idhini kuepuka kuondolewa mara kwa mara pindi halmashauri zinapo badili matumizi ya maeneo,amesema.
Mafunzo hayo ya Viongozi wa shirikisho la umoja wa Machinga Tanzania yameandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya jamii,Jinsia,wanawake na makundi maalumu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo huku kaulimbiu yake ikiwa "Machinga ni fursa sahihi ya kukuza uchumi wa nchi yetu".
0 Comments