Ticker

6/recent/ticker-posts

RAIS MWINYI MGENI RASMI WIKI YA MAKISATU 2022



*********

Na Zena Mohamed,Dodoma.

RAIS wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt.Hussen Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa wiki ya ubunifu na mashindano ya kitaifa ya sayansi, Teknolojia na ubunifu (MAKISATU)itakayoanza Mei 15 hadi Mei 20,2022 Jijini Dodoma .

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo,Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda kuhusu kuanza kwa maadhimisho hayo amesema kuwa mashindano hayo yataibua, kutambua, kuadhimisha, kujenga, kukuza na kuendeleza ubunifu wa Watanzania katika nyanja za Sayansi na Teknolojia ili kuchangia juhudi za maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Amefafanua kuwa Rais Mwinyi atazindua rasmi maadhimisho hayo Mei 16 huku Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango akitarajiwa kufunga maadhimisho hayo Mei 19 mwaka huu.

Ameeleza kuwa maadhimisho ya wiki ya MAKISATU ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya awamu ya sita ya kuongeza hamasa ya matumizi ya sayansi na kwamba maadhimisho hayo yatafanyika katika ngazi ya Mikoa na Taifa.

Ametaja Mikoa iliyofanikiwa kuandaa maadhimisho ya wiki ya ubunifu kwa mwaka huu ni pamoja na Dar es Salaam,Dodoma,Mbeya,Arusha,Iringa,Mwanza,Zanzibar,Tanga,Kilimanjaro,Morogoro,Njombe,Kagera,Mtwara,Kigoma,Mara na Ruvuma.

"Katika ngazi ya mikoa maadhimisho haya yanaratibiwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya hii,COSTECH na programu ya FUNGUO chini ya Shirika la UNDP kupitia kumbi za ubunifu,vituo vya ubunifu,taasisi za umma na binafsi Katika mikoa husika ambapo uratibu huu inahusisha Ofisi ya Rais-TAMISEMI kupitia maafisa maendeleo ya jamii,"amesema

Amesema Katika ngazi zote mbili,mikoa na Taifa, MAKISATU yataambatana na matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilele chake yatakayolenga kupata washindi Kwa mwaka 2022 Katika ngazi ya kitaifa,majukwaa ya majadiliano kuhusu maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na ubunifu nchini yanayohusisha utafiti na ubunifu.

"Mashindano haya pia yatahusisha Serikali na wadau mbalimbali wa ubunifu na maendeleo ndani na nje ya nchi Kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja katika kuhamasisha maendeleo na matumizi ya teknolojia kwa maendeleo ya uchumi na jamii,"amesema.

Amebainisha kuwa katika maadhimisho hayo pia kutakuwa na mafunzo na semina kwa wabunifu ikiwemo elimu na ujasiriamali.

Kutokana na hayo Waziri huyo mwenye dhamana ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

ametumia nafasi hiyo kuwataka wabunifu na wananchi wote kushiriki katika maadhimisho hayo na kuendelea kutumia bunifu mbalimbali zinazotokana na watanzania katika shughuli za maendeleo.

Wiki hiyo pamoja na mambo mengine Kwa mwaka huu imebeba kaulimbiu ya "Ubunifu kwa maendeleo endelevu".

Post a Comment

0 Comments