***********************
MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amekagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Veta kinachojengwa Wilayani Ikungi na kuridhishwa na kasi inayoendelea.
Aidha,ametoa ombi kwa uongozi wa VETA kuwa chuo hicho kitakapokamilika pamoja na ujuzi wa fani mbalimbali za ufundi zinazotolewa,waone namna ya kuingiza mtaala wa Elimu ya kilimo na ufugaji.
Ziara hiyo ameifanya Mei 15,2022,ikiwa ni utaratibu wake aliojiwekea wa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayojengwa katika jambo lake.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo,Mtaturu amesema chuo hicho ni muhimu katika kuchochea uchumi wa wananchi wa jimbo hilo na kwamba serikali ilishawapatia jumla ya Shilingi Bilioni 2.4 kugharimia ujenzi huo.
"Nimshukuru sana Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia fedha za ujenzi wa chuo hiki kwenye wilaya yetu ambao ni mradi muhimu,na chuo hiki kikikamilika kitawasaidia vijana wetu kupata elimu ya ufundi ili kujiandaa kujiajiri na kujihakikishia kipato chao,"amesema.
Amesema uwepo wa mtaala wa kilimo na ufugaji utawasaidia kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kuboresha shughuli zao wanazofanya.
"Ushauri huu tulioutoa wabunge tukiwa bungeni,na Waziri wa Elimu Prof Adolf Mkenda alilipokea na kuahidi kulifanyia kazi,"ameongeza.
Akitoa taarifa mbele ya mbunge,msimamizi wa ujenzi John Thomas amesema kwa sasa majengo ya fani za magari, umeme, ujenzi, ushonaji,kompyuta na bwalo la chakula yapo kwenye hatua za upauaji .
"Jengo la utawala na hosteli za wavulana na wasichana yapo hatua ya kupandisha boma,"amesema.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Unyahati kinapojengwa chuo hicho Abeli Surri amemshukuru sana mhe mbunge kwa kuwasemea bungeni wananchi wa Singida Mashariki kwani kupitia miradi mingi inayotekelezwa .
"Sisi wananchi wenzako tunakushukuru sana,umekuwa mdomo wetu bungeni,umesaidia kusukuma utekelezaji wa miradi mingi kupitia michango na maswali yako bungeni,tunakushukuru sana,"ameshukuru.
Ujenzi wa chuo hicho unatarajiwa kukamilika mwezi August mwaka huu.
0 Comments