Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele, akiwahamasisha wanafunzi kujiunga na kujiwekea akiba NSSF.
Meneja wa NSSF Mkoa wa Temeke, Feruzi Mtika.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya, Mhe. Suma Fyandomo.
Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Mhe. Joseph Tadayo, akieleza umuhimu wa kujiwekea akiba kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.
Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Khadija Shaaban Taya "Keisha"
Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kigoma,Mhe. Zainab Katimba.
Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Saraphina akitoa buradani ya nguvu wakati wa kampeni ya "Boom Vibe na NSSF" iliyofanyika Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM)
Wanafunzi wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na IFM wakijiunga na NSSF kupitia Mpango wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi.
Wanafunzi wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na IFM wakifuatilia mada mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya wabunge ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria.
***
Na Mwandishi Wetu
Mamia ya wanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni na Chuo cha Usimamizi wa Fedha cha IFM, wamejiunga na kujiwekea akiba na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) baada ya kupata elimu ya Hifadhi ya Jamii kuhusu umuhimu wa kujiunga na kujiwekea akiba kwa maisha ya sasa na baadaye.
Elimu hiyo ya hifadhi ya jamii ilitolewa kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki kupitia kampeni ya “Boom Vibes na NSSF” iliyoongozwa na baadhi ya wabunge kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria akiwemo Mhe. Khadija Shaaban Taya “Keisha”, Mhe. Suma Fyandomo, Mhe. Zainab Katimba na Mhe. Joseph Tadayo.
Akizungumzia na wanafunzi wa vyuo hivyo kwa nyakati tofauti Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele alisema kampeni hiyo ina lengo la kutoa elimu ya Hifadhi ya Jamii kwa wanafunzi wanaosoma elimu ya juu wakiwemo wa vyuo hivyo kuhusu umuhimu wa kujiwekea akiba kwa kujiunga na kuchangia katika Mfuko kupitia Mpango wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi.
Kwa upande wa Meneja wa NSSF Temeke, Feruzi Mtika alisema Mfuko umedhamiria kukutana na wanafunzi wa elimu ya juu ili kuwahamasisha namna bora ya kujiwekea akiba kwa manufaa yao ya sasa na baadaye kwani hifadhi ya jamii inamsaidia mtu kukabiliana na majanga mbalimbali pale uwezo wa kufanya kazi unapopungua kwa uzee au ugonjwa.
Alisema Mfuko umeweka utaratibu nzuri wa kujichangia kwa wanachama wa sekta isiyo rasmi au watu binafsi wanaofanya shughuli za halali ambao wanaweza kuchangia kidogo kidogo ili mradi mwisho wa mwezi wawe wametimiza shilingi 20,000 au zaidi kwa kutumia simu ya mkononi kupitia namba ya kumbukumbu ya malipo “Control number”.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wabunge hao waliweka msisitizo mkubwa kwa wanafunzi wa elimu ya juu kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba kwa kujiunga na NSSF kwani hawatajutia uamuzi huo.
Mhe. Zainab Katimba ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kigoma, aliwahamasisha wanafunzi hao kujiwekea akiba kwa kuchangia shilingi 20,000 kwa mwezi ambayo itawafaa baada ya kumaliza chuo kwa kupata mtaji nzuri wa kuanzia maisha huku wakiendelea kujichangia.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Mhe. Joseph Tadayo alisema mtu anakuwa nacho sio kwa anachoingiza bali kwa kile anachoweka hivyo aliwasihi wanavyuo kujenga utamaduni bora wa kujiwekea akiba ambayo itawasaidia baadaye.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Khadija Shaaban Taya ‘Keisha’ aliwataka wanafunzi hao kuchangamkia fursa ya elimu ya hifadhi ya jamii waliyopata kwa kujiwekea akiba ambayo ndio msingi wa kesho iliyo njema.
“Nataka niwaambieni nilianza kuchoma maandazi na chapati lakini kile nilichokuwa napata nilikuwa najichangia NSSF ambapo nilipata kama shilingi milioni tatu na kufungua duka hadi sasa nina biashara nyingi na naendelea kuchangia NSSF hivyo na nyinyi mchangamkieni fursa hiyo,” alisema Mhe. Suma Fyandomo ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya
0 Comments