Ticker

6/recent/ticker-posts

JAJI MSTAAFU DAVID MRANGO AAGWA KITAALUMA

Na James Kapele na Mayanga Someke, Mahakama-Sumbawanga

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani leo tarehe 27 Mei, 2022 ameongoza jopo la baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu katika hafla maalum ya kumuaga kitaaluma Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. David Mrango aliyestaafu katika utumishi wa umma tarehe 02 Januari 2021.

Akizungumza katika hafla hiyo mahsusi ya kuagwa kitaaluma kwa Jaji Mrango, iliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Jaji Kiongozi, Mhe. Siyani amemshukuru kwa utumishi wake na kuahidi kuyaenzi yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake.

Naye, Jaji Mstaafu, Mhe. David Mrango amemshukuru Mungu kwa kufikia hatua ya kustaafu kwani kazi hii ilikuwa na ugumu wake, amewashukuru pia watumishi wa Mahakama kwa kumuwezesha kufanya kazi yake vizuri.

“Katika muda wangu wa kazi ndani ya Mahakama nimegundua kuwa Wahe. Majaji na Mahakimu hawawezi kufanya kazi zao kwa ufanisi bila uwepo wa Makarani, Watendaji, Wahudumu wa Ofisi, Madereva na hata Walinzi,” amesema Mhe. Mrango.

Akiendesha shauri dogo maalum lililofunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga na kupewa namba 1/2022, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani alipokea hotuba nne ambazo zimezungumzia safari ya maisha ya kitaaluma ya Jaji Mstaafu, Mhe. Mrango.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dunstan Ndunguru amesema Mhe. Mrango ameacha alama ya kuigwa kwa watumishi wote kwani alihakikisha malengo katika mpango mkakati wa Mahakama yanatekelezeka ipasavyo.

“Mh. Jaji Mrango alikuwa mara nyingi akisisitiza usikilizwaji wa mashauri kwa haki na kufuata taratibu hasa kwa watuhumiwa ambao ni wananchi wa kawaida (laymen) wasiojua sheria na taratibu za kiufundi,” amesema Jaji Ndunguru.

Awali akiwasilisha hotuba ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Simon Peres ambaye ni Mwendesha Mashtaka wa Serikali mkoa wa Rukwa pamoja na mambo mengine amesema Mhe, Jaji Mstaafu David Mrango ni moja ya Majaji ambao tasnia ya sheria itamkumbuka kwa kuwa ameacha misingi mizuri katika wigo wa sheria huku akitoa mfano wa shauri moja ambalo Mhe.Mrango ameacha alama katika wigo wa sheria shauri la ‘Saimon S/O Maduhu @Buhalo & 4 others, Crim. Appeal No. 10 of 2020.’

Katika shauri hili Mhe, Mrango alitoa hukumu kwa kusema “It is a principle of law that in any criminal proceedings it is the charge which lays a foundation of trial. As such the charge must contain sufficient information to enable the appellant to understand the nature of charge he faces and what defence to put up”. Ametaja pia mashauri mengine mengi ambayo Mhe. Mrango ameyatolea uamuzi.

Naye Wakili wa Kujitegemea aliyesoma hotuba kwa niaba ya Chama Cha Mawakili Tanzania katika Tawi la Mbeya, Wakili Bartazar Chambi pamoja na mambo mengine ametoa wasifu wa maisha ya utumishi wa Mhe. Mrango huku akisisitiza kwamba, katika utumishi wake wa umma Jaji Mrango alikuwa ni mtu wa kujali muda na kusimamia maadili ya watumishi wa Mahakama kwa ujumla.

Wakili Chambi ameongeza kuwa, Mhe. Mrango aliilinda kwa dhati taaluma ya sheria kwani hakutaka itumike vibaya na watu wasio na taaluma hiyo. “Akiwa Sumbawanga alidhibiti vishoka na mmoja wa vishoka hao ajulikanaye kwa jina la Mwakasege alifungwa gerezani.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Watumishi wa Kanda hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Sebastian Waryuba aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Chama cha Mawakili wa kujitegemea Tawi la Mbeya na wageni wengine.

Katika hatua nyingine, Jaji Kiongozi, Mhe. Siyani alipata fursa ya kuzungumza na Watumishi wa Mahakama katika Kanda hiyo ambapo amesisitiza kuzingatia mambo makuu matatu ambayo ni maadili na uadilifu katika kazi, Kanda kujiwekea mpango mkakati katika masuala ya kupunguza mlundikano wa mashauri pamoja na matumizi ya TEHAMA na ushirikiano katika utendaji wa kazi kwa watumishi wa ngazi zote.

Baada ya kikao hicho, Watumishi wa hiyo wamempongeza, Mhe. Siyani kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kumtakia heri na baraka katika utendaji kazi wake.





Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama. Walioketi wa tatu kulia ni Mhe. David Mrango, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania (aliyeagwa kitaaluma), wa pili kushoto ni Mhe.John Mgetta, Jaji wa Mahakama Kuu-Masjala Kuu, wa tatu kushoto ni Mhe. Dunstan Ndunguru, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, wa pili kulia ni Mhe.Filmin Matogoro, Jaji wa Mahakama Kuu- Kanda ya Iringa, wa kwanza kulia ni Mhe. James Karayemaha, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na wa tatu kushoto ni Mhe. John Nkwabi, Jaji wa Mahakama Kuu- Kanda ya Sumbawanga.


Shauri dogo maalum la kumuaga kitaaluma Mhe. David Mrango, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu likiendelea kusikilizwa.




Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akiwasalimia watumishi wa Mahakama Kanda ya Sumbawanga alipowasili katika Mahakama hiyo kwa ajili ya kuongoza hafla maalum ya kumuaga kitaaluma Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Mhe. David Mrango. Aliyesimama kushoto kwake ni Mhe. Dunstan Ndunguru, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Sumbawanga.




Mhe. Siyani akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga.

Post a Comment

0 Comments