Ticker

6/recent/ticker-posts

HAPPINESS LUSHINGE; MWANAMKE PEKEE ANAYEENDESHA MITAMBO YA KUCHIMBA MADINI KUPITIA CHINI YA ARDHI

 

Happiness Lushinge akiwa na cheti chake cha Tuzo ya Mfanyakazi bora
***

Kwa muda mrefu sekta ya Madini nchini imekuwa ikitawaliwa na ajira nyingi za Wanaume na kuwepo dhana kwamba Wanawake hawaziwezi kazi ngumu za migodini. Happiness Lushinge, mfanyakazi wa Mgodi wa Barrick North Mara, anayeendesha mitambo mikubwa ya uchimbaji wa Madini inayopita chini ya ardhi, amedhihirisha kuwa Wanawake wanaweza kumudu kufanya kazi ambazo nyingi zanafanywa na Wanaume.

Katika mahojiano hivi karibuni, Lushinge, alisema alijiunga na North Mara, mnamo 2014, kama mhudumu wa usafi baada ya kuhitimu sekondari na masomo ya Maarifa ya Nyumbani. Kila wakati aliota kuwa maisha mazuri yajayo yalikuwa mbele yake. Kufikia mwisho wa 2020, ndoto yake ilitimia alipoajiriwa kama deeva wa mashine za uchimbaji za chini ya ardhi akiwa Mwanamke wa kwanza na pekee kuifanya kazi hii mgodini hapo.

“Mwanzoni nilikuwa siamini kama ni mimi naweza kuendesha mitambo mikubwa ya uchimbaji nikiwa mwanamke pekee miongoni mwa wafanyakazi wenzangu wanaume. Nimetokea kumudu kazi yangu vizuri mpaka naaminiwa na wasimamizi wangu kutokana na kuchapa kazi vizuri, kufuata taratibu na kuhakikisha malengo yaliyowekwa na mwajiri wangu yanafikiwa,” alisema Lushinge.

Anasema amefurahi kuona katika kipindi kifupi kazini cha mwaka 1 katika jukumu lake jipya, ametangazwa kuwa Mfanyakazi Bora wa Mwaka wa Mgodi wa North Mara kwa 2021, hatua ambayo alidai imezidi kumpa moyo wa kujifunza zaidi kuendesha mitambo mingine ya kisasa ya uchimbaji wa madini.

Alipoulizwa siri kubwa ya mafanikio hayo, alisema yanatokana na kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wafanyakazi wenzake ambao wamempatia mafunzo pia kampuni imekuwa ikiandaa mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo wake ambayo yamemsaidia katika safari yake ya mafanikio.

Pia alisema kuwa sera za mwajiri wake ya kutoa fursa kwa Wanawake sawa na Wanaume katika kazi za migodini zimemwezesha kusonga mbele kwa kujiamini, anajivunia kuona mchango wake wa kazi unathaminiwa wakati wote.” Nafurahi kuona wafanyakazi Wanawake tuko wengi kwenye kampuni kwenye vitengo na fani mbalimbali wengine wakiwa wanafanya kazi za kitaalamu kama Wahandisi na nafasi za juu za uongozi”, alisema.

Vilevile aliongeza kuwa uwekezaji mkubwa wa Barrick, kwenye matumizi ya teknolojia za kisasa za kimataifa kwenye migodi yake, kumemwezesha kujua mambo mengi hususani kuhusiana na uendeshaji wa mitambo ya uchimbaji wa chini ya ardhi.

Kuhusu changamoto anazokumbana nazo katika kazi yake, alisema ni za kawaida kwa kuwa hakuna kazi yoyote isiyokuwa na changamoto.

Happiness, alitoa wito kwa wasichana waliopo mashuleni kuchangamkia masomo yanayohusiana na fani ya madini ili wasiachwe nyuma katika fursa mbalimbali zinazotokea na watambue kuwa hakuna kazi wanayoifanya Wanaume ambayo Wanawake hawawezi kuifanya.

Kuhusu malengo yake ya baadaye, alisema anataka kujifunza kuendesha mashine mbalimbali za uchimbaji ili aweze kufikia viwango vya kuwa Mwendeshaji wa kimataifa, “unajua hapa migodini matumizi ya teknolojia za kisasa ndio mahali pake hivyo ili usibaki nyuma inabidi kuendelea kujifunza mambo mapya hasa matumizi ya vifaa vya uchimbaji vya teknolojia ya kisasa.

Alipoulizwa anatumia vipi muda wake wa mapumziko, alisema anapendelea kukaa na familia yake, kusoma vitabu na kufanya mazoezi.

Akiongelea utendaji wa kazi wa Happiness, Mkuu wake wa idara anayofanyia kazi.Asha Mambo, alisema ni Mfanyakazi mwenye bidii, mchapakazi, mwenye kuzingatia usalama kazini pia ni mwepesi wa kujifunza ambaye kwa muda mfupi aliofanya kazi amedhihirisha kuwa na uwezo mkubwa kiasi cha Kampuni kujivunia kuwa naye.


Post a Comment

0 Comments