Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk.Jabiri Bakari akizungumza na waandishi wa habari kihusiana na hali ya gharama za Data kwa watumiaji wa mawasiliano , jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk.Emmanuel Manase akitoa mada namna ya gharama za data zinavyokwenda nchini jijini Dar es Salaam.
Watendaji wa TCRA na Waandishi wa habari wakifatilia mada wakati mkutano wa waandishi habari kuhusiana na Data.
******************
*Tanzania ina bei za chini ya Data kwa ukanda wa SADC na Afrika Mashariki.
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetaja mabadiliko ya teknolojia na kwa gharama za data Tanzania iko chini kwa ukanda wa Jumuiya ya nchi zilizo Kusini Mwa Jangwa la Sahara na Ukanda wa Afrika mashariki.
Kupanda kwa gharama za matumizi ya Data za Internet kunatokana na mabadiliko ya uwekezaji wa miundombinu mbalimbali katika sekta ya mawasiliano lakini watoa huduma wameendelea kutoa huduma kulingana na matakwa ya kisheria na kufatiliwa na mamlaka ya udhibiti TCRA
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta TCRA, Dk. Emmanuel Manase alisema kuwa vifaa vya mawasiliano vinatengenezwa na kampuni chache duniani na kwamba bei ya vifaa hivyo, haiangalii uchumi wa nchi husika.
Alisema gharama za data mpaka Aprili mwaka huu ni kutoka Sh 1.67 hadi 2.60 huku bei ya data ikiwa Sh 1.5 kwa Megabaiti (Mb) hadi Sh 9.35 kwa Mb.
Dk. Manase amesema kuwa ili watanzania wote waweze kupata huduma hizo za data, uwekezaji mkubwa unahitajika ili nchi nzima ipate mawasiliano bila kujali uchumi na idadi ya watu.
"Stadi za TCRA zimeonesha kuwa gharama halisi za kuuza data ni kati ya Sh 2.03 Mb ambazo mtoa huduma anaweza kuuza na kurudisha gharama za uendeshaji na Sh 9.35 Mb ni ambazo mtoa huduma anaweza kuendeleza uwekezaji," alisema.
Alisema sababu za kuisha kwa haraka kwa data ni kubadilika kwa teknolojia ikiwemo Kasi na muda unaotumika kupakua na kupakia data, ubora wa vifaa vya teknolojia na kuongezeka kwa ukubwa wa picha.
Alisema mamlaka hiyo imekuwa ikifuatilia vifurushi vyote vinavyoenda sokoni na kwamba mteja hununua kulingana na mahitaji yake.
Alisema bei ya huduma za data kwa nchi za Afrika Mashariki, wastani wa gharama nchini ni Dola za Marekani 0.75 kwa Gb moja sawa na Sh 1,725 ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi sita kati ya 52 zenye gharama nafuu za data.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabir Bakari alisema kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikifuatilia kuhusu mabadiliko ya vifurushi na kubaini kuwa hakuna tatizo.
"Vifurushi vilivyopo ni sahihi kwani sio mara zote vinapanda kwa sababu kila baada ya miezi mitatu mtoa huduma hutakiwa kutoa taarifa kama amebadilisha huduma hiyo vipo vipya, vinavyoshuka, kubaki au kuondoka kabisa kwenye soko. Kila mabadiliko yanapotokea teknolojia huangalia utaratibu na matumizi ya vifurushi hivyo," alisema Dk. Bakari.
0 Comments