Celina Gombanillah
**
Kufanya kazi ya Uuguzi kunahitaji kuwa na moyo wa kujituma na kujitolea, pamoja na kusomea taaluma hiyo bado Wauguzi wanapokuwa kazini mbali na kuwasaidia wagonjwa kupata huduma za kiafya bado wanakumbana na kazi mbalimbali nje ya majukumu yao ya kikazi ambazo wanazitekeleza kuhakikisha wagonjwa wako katika hali nzuri.
Celina Gombanillah, Muuguzi wa Zahanati iliyopo katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick Bulyanhulu, anaamini kuwa kusaidia watu ni wito wake. "Ikiwa kuna kazi ambayo inahitaji mtu kutumia viwango vya juu vya taaluma na kuifanya kwa weredi wakati wote, basi ni uuguzi kwa sababu inahusisha kuokoa maisha," Celina anasema.
Katika mahojiano hivi karibuni, Gombanillah, alisema alijiunga na Kampuni ya Barrick, katika Mgodi wa Bunyanhulu, mnamo mwaka 2011, kabla ya hapo alifanya kazi hiyo ya uuguzi katika kituo cha afya cha Mgodi wa kampuni ya Madini ya Mwadui , baada ya kuhitimu mafunzo ya stashahada ya uuguzi katika Chuo cha Nkinga kilichopo wilayani Igunga, mkoani Tabora.
“Kwenye maeneo ya Migodi nimeweza kukutana na watu wengi kutoka Mataifa mbalimbali ambapo nimejifunza mambo mengi kuhusiana na fani yangu kuendana na viwango vya juu vya utendaji kazi vilivyopo kwenye makampuni yanayomiliki migodi. Namudu vizuri kazi yangu na kufuata taratibu sambamba na kuhakikisha malengo na matarajio yaliyowekwa na mwajiri wangu yanafikiwa,” alisema Gombanillah.
Anasema amefurahi mchango wake wa kazi unathaminiwa na kampuni ambapo mwaka jana alipata tuzo kwa kutangazwa kuwa kuwa Mfanyakazi Bora wa Mwaka wa Mgodi wa Bulyangulu kwa 2021, hatua ambayo alidai imezidi kumpa moyo wa kufanya kazi yake kwa bidii zaidi.
Alipoulizwa siri kubwa ya mafanikio hayo, alisema yanatokana na kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wafanyakazi wenzake ambao wakati wote wamekuwa wakimpatia ushirikiano mkubwa pia kampuni imekuwa ikiandaa mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo anadai yamemsaidia katika safari yake ya mafanikio.
Pia alisema anavutiwa na sera za mwajiri wake za kutoa fursa kwa Wanawake sawa na Wanaume katika kazi za migodini . "Nafurahi kuona idadi ya wafanyakazi Wanawake kwenye migodi inazidi kuongezeka, ukitembelea migodi unakuta Wanawake wakifanya kazi kwenye vitengo mbalimbali vikiwemo vya Uhandisi na Jiolojia.Kwenye nafasi za Uongozi pia kuna idadi kubwa ya Wanawake” alisema Celina.
Vile vile aliongeza kuwa uwekezaji mkubwa wa Barrick, kwenye matumizi ya teknolojia za kisasa za kimataifa kwenye migodi yake, kumemwezesha kujua mambo mengi ya matumizi ya vifaa vya tiba vya kisasa na kujenga mazingira bora ya kufanyia kazi yenye viwango vya juu vya kimataifa.
Kuhusu changamoto anazokumbana nazo katika kazi yake,alisema ni za kawaida kwa kuwa hakuna kazi yoyote isiyokuwa na changamoto.”Changamoto kwangu huwa nazichukulia kama ni sehemu ya kujifunza mambo mapya” alisema.
Celina alitoa wito kwa Wauguzi wenzake na wote wanaotaka kusomea fani hiyo kuhakikisha wanakuwa na weledi katika fani hiyo pia wanafanya kazi kwa umakini na ufanisi wakati wote ili kukidhi matakwa ya wagonjwa wanaotegemea kupata huduma nzuri kutoka kwao.
Akiongelea uchapakazi wake, Mkuu wa idara anayofanyia kazi, Dk. Said Kudra, alisema kuwa Celina ni mfanyakazi anayetegemewa kutokana na kujituma na kufanya kazi yake kwa weredi mkubwa ambaye yuko tayari wakati wowote kuhudumia wagonjwa hata baada ya muda wa saa za kazi.
Kuhusiana na malengo yake ya baadaye alisema anataka kujiendeleza zaidi kitaaluma ili aendelee kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa.
0 Comments