Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima alionesha moja ya kisima cha maji kilichochimbwa katika eneo la ujenzi ambacho kitasaidia kwa matumizi ya binadamu.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima alifafanua maelezo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Dr Pindi Chana, kushoto ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa hifadhi ya Ngorongoro Joshua Mwankunda.
***************
Na Hamida Kamchalla, HANDENI.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dr. Pindi Chana amesema wananchi wanaotakiwa kuondoka kwenye hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha ambao wako tayari kwa hiyari waende wakajiandikishe ili kuweza kupatiwa makazi ya kudumu katika kijiji cha Msomela wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.
Waziri huyo ameyasema hayo jana alipotembelea kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba hizo za kudumu kwa wananchi hao ambapo watapatiwa maeneo ya kufugia mifugo yao ambayo watahamishwa nayo kutoka hifadhi ya Ngorongoro wanapoishi na kutakuwa kuondoka kupisha hifadhi hiyo baada ya uharibifu mkubwa uliosababishwa na wanyama pamoja na shuhuli za kibinadamu.
Chana amesema milango iko wazi kwa wale wote wanaotaka kuhama na tayari nyumba takribani 100 zimeshajengwa wilayani Handeni na serikali iko kwenye michakato mbalimbali ya kukamilisha huduma za kijamii, ikiwemo miundombinu ya barabara, maji na umeme.
"Ujenzi wa nyumba unaendelea, tuna awamu ya kwanza na ya pili, na hivi sasa tuna nyumba zisizopungua 100 ambazo tayari zimekamilika, fursa hii siyo rahisi kuipata na ni muhimu sana kwa wale ambao wamejiandikisha, lakini wale ambao nao wako tayari kujiandikisha kwa hiyari milango iko wazi na kuanzia sasa kaya mbalimbali zitaingia hapa Msomela" amesema.
Chana amewahakikishia na kuwatoa hofu wananchi hao lakini pia kupongeza uongozi wa Mkoa na Wilaya pamoja na wananchi wa kijiji hicho kwa imani kwa kujitolea na kuhakikisha ujenzi huo unakwenda kama ilivyokusudiwa na kuwataka wenyeji hao kuwapa ushirikiano pindi watakapowasili.
"Napenda niutangazie umma kwamba, tunao ndugu zetu wanaotaka kuhamia hapa, na takwimu kila siku zinaongezeka, hapa naomba niweke msisitizo, lengo la kunusuru eneo lile la urithi wa Taifa kwa kizazi hiki na kunachokuja, uhakika wa eneo la kuishi, malisho pamoja na nyumba, hili ni jambo jema sana serikali iketenda kwa wananchi wake" alisema.
"Lakini pia lengo la wenzetu wale kuhamia hapa tunataka waishi maisha bora ya Mtanzania, muendelee kuwapokea na ninaagiza halmashauri ya Wilaya ya Handeni, zile asilimia 10 za vijana, wakina mama na wenye ulemavu, zitengwe na wakifika hapa wawezeshwe waanze ujasiriamali na shuhuli mbalimbali ili maisha yao yawe bora" aliongeza.
Naye mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima amesema wamepokea maagizo ya Rais, na jambo kubwa la wizara ya Maliasili na Utalii ni kuinusuru hifadhi hiyo na serikali ili kupunguza nguvu ya mifugo na uharibifu wa rasilimali kuu ya Taifa ambayo pia ni urithi kwa dunia.
"Kwahiyo wajibu wetu sisi ni kuinusuru Ngorongoro lakini wakati huohuo kuhakikisha kwamba hawa Watanzania wenzetu waliokuwa wamekaa pale muda wote na sasa wamejikuta kwenye mazingira ambayo hifadhi imeharibika kwa uwepo wa mifugo iliyopo kwa kiasi kikubwa, tunawaleta hapa na sisi tuliopo tukahakikisha kwamba hatuwatoi kule na kuua kuwatupa" alisema Malima.
Malima amefafanua kwamba serikali imetengeneza utaratibu wa Mkoa pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama wanasimamia zoezi hilo kuhakikisha kwamba makazi ya awali ya nyumba 300 hadi 400 zinamalizika kwa ajili ya familia zunazokuja na mifugo yao.
Amesema eneo hilo limepewa hadhi ya kitongoni ambacho wananchi wenyeji wamekipa jina la 'Orormoti' kimezungukwa na vijiji vinne vya Msomela, Mzeri, Kwababu na Kibaya upande wa Kiteto ambavyo vyote vina huduma muhimu za kijamii.
"Hayo ndiyo mambo muhimu ambayo sasa hivi tunapambana nayo, kuna zahanati Msomelo ambayo tunataka kuipandisha hadhi na kuwa kituo cha afya kwa ajili ya kuboresha huduma, fedha zimeshatengwa na zoezi hili tunalisimamia sisi pamoja na wenzetu wa Ngorongoro ili wenzetu wakija wakute tayari ujenzi huo unakamilika" alisema.
"Kuna shule ya msingi inaongezwa vyumba vya madarasa 6 na shule ya sekondari tunaongeza vyumba 12 vya madarasa kwa ajili ya kukidha wingi wa wanafunzi, lakini pia kuna mradi wa maji, visima virefu vimechimbwa na maji yamepatikana na tayari umeme uko kijiji cha jirani unakaribia kuingia hapa" aliongeza Malima.
Picha 10 jpg.. Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima alionesha moja ya kisima cha maji kilichochimbwa katika eneo la ujenzi ambacho kitasaidia kwa matumizi ya binadamu.
Picha 06 jpg.. Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima alifafanua maelezo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Dr Pindi Chana, kushoto ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa hifadhi ya Ngorongoro Joshua Mwankunda
0 Comments